Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,Dar
SERIKALI imepongeza kampeni inayofanywa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) katika kupambana na ukatili wa kijinsia na udhalilishaji sehemu za kazi.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi na Ajira), Jenister Mhagama.
Alikuwa akizungumza akifungua kongamano la wadau kuhusu ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake maeneo ya kazi ambapo kauli mbiu ilikuwa ‘uwajibikaji kutokomeza na udhalilishaji mahali pakazi’.
Waziri Mhagama unyanyasaji umekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hivyo mashirika kama WiLDAF yanayopinga ukatili yatanastahili kupongezwa.
“Serikali yetu chini ya mama jasiri na shupavu Rais Samia Suluhu Hassan inatambua na imeamua kuhakikisha inawalinda wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia na tutafanyakazi hiyo kwa nguvu zetu zote,’ alisema Mhagama
“Kwenye hili kongamano mmesema ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wenu unaosema wanawake na ajira na lengo ikiwa ni kuboresha mazingira mazuri ili wanawake waweze kushiriki katika shughuli za uchumi wa viwanda tunawapongeza sana,” amesema Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema mradi huo unaendana na dhana nzima ya Rais Samia ambaye ameamua kuwa balozi wa wanawake kwa kutekeleza kwa vitendo usawa wa kijinsia kwa kuona umhimu wa wanawake kushiriki katika ujenzi wa uchumi.
Waziri Mhagama amesema Rais Samia amevunja miiko iliyokuwepo tangu Uhuru kwani zipo nafasi ambazo awali zilikuwa zikionekna kama za wanaume na wanawake hawapaswi kuzishika.
Ametoa mfano kuwa hatua ya Rais Samia kumteua aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC), Dk. Stegomena Tx imeibua shangwe kubwa miongoni mwa wanawake.
“Tangu Uhuru hatujawahi kuona Waziri wa Ulinzi mwanamke na sisi wanawake tulishazoea na kuona hiyo ni hali ya kawaida kabisa kumbe si kweli kwamba ni ya wanaume,” amesema
Amesema chaguo la Dkt. Stegomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi ni sahihi kwani amefanyakazi kubwa sana SADC na ana uzoefu wa kutosha kabisa kuongoza hiyo wizara.
Ameshukuru WiLDAF kwa harakati zake za kutetea maendeleo ya wanawake akisema kwamba hata mafanikio yake kwenye siasa asasi hiyo imetoa mchango mkubwa.
Mwenyekiti wa WiLDAF, Monica Mhoja amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili ukatili na udhalilishaji wa wanawake katika sekta ya kazi na ajira.
Amesema lengo lingine ni kupendekeza mbinu na kuandaa mpango mkakati wa pamoja katika kuondoa changamoto zilizopo kwa wanawake sehemu za kazi.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato