November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri, Katibu Mkuu kushiriki kilele cha Sauti za Busara

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa leo anatarajia kushiriki kwenye kilele cha Tamasha la kimataifa la Sauti za Busara, Zanzibar.

Tamasha la Sauti za Busara ni miongoni mwa matamasha makubwa nchini ambayo yamefanikiwa kuonesha utamaduni wa nchi Tanzania duniani kupitia Sanaa za muziki.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt, Hassan Abbasi ambaye anashiriki amesema tamasha la mwaka huu limeboreshwa zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Aidha, amesema kutokana na tamasha hili amejifunza mengi ambayo yanaweza kusaidia kuboresha matamasha yanayokwenda kuandaliwa hivi karibuni.

“Tumejifunza mengi katika tamasha hili, tutatumia, kazi iliyombele yetu ni kubeba mambo mazuri ya tamasha hili kuboresha matamasha yanakuja mbele yetu yawe kwenye hadhi ya kimataifa ili kuitangaza Tanzania na kuuza utamaduni wetu duniani kama tulivyo elekezwa na Rais wetu kipenzi, Mhe. Samia Suluhu Hassan”. Ameongeza Dk. Abbasi

Pia katika tamasha hili Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Dkt. Emmanuel Ishengoma ameshiriki.

Awali Rais Samia katika tamasha la utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro alielekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na wadau kuandaa matamasha makubwa ambayo yatasaidia kutangaza utalii na utamaduni wa Taifa la Tanzania kimataifa.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar. Dkt. Hussein Alli Mwinyi ameliezea Tamasha la Sauti za Busara kuwa lina mchango muhimu wa kuhamasisha umoja na mshikamano nchini.