November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mchengerwa aelekeza mchakato wa Ajira zote serikalini uratibiwe na sekretarieti ya Ajira

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa ameelekeza mchakato wa ajira katika taasisi zote za umma nchini uratibiwe na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kama chombo huru ili kuleta uwazi na kuwezesha haki kutendeka.

Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliyopewa dhamana ya kusimamia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.

Mchengerwa amesema amelazimika kutoa maelekezo hayo kwasababu hivi karibuni baadhi ya waajiri wamekuwa wakiomba vibali vya ajira na kutaka kuendesha mchakato wa ajira wao wenyewe katika taasisi zao hali inayoondoa uwazi, ushindani na usawa katika kuendesha mchakato wa ajira.

Amesema lengo la Serikali ni kuondoa upendeleo unaotokana na undugu, ukabila, udini na masuala mengine yasiyo ya kimaadili katika mchakato wa ajira kwenye Utumishi wa Umma.

“Utakuta baadhi ya taasisi, watumishi wake wameajiriwa kindugu, kidini na kikabila, nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kusimamia utendaji kazi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ninataka tuondokane na changamoto hiyo ili twende kwenye uwazi na haki katika mchakato wa ajira Serikalini kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mchengerwa amesema baada ya maelekezo aliyoyatoa, hategemei kusikia taasisi yoyote ya umma inafanya mchakato wa ajira bila kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Aidha, Mchengerwa amewataka Wajumbe wa Bodi aliyoizindua, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi kwani wameaminiwa na Serikali na ndio maana wakapewa nafasi hizo ili kuisaidia Serikali kupata watumishi wenye uwezo ambao watatoa mchango kwa maendeleo ya taifa.

Akitoa neno la Shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bibi Sophia Kaduma amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo na Mhe. Mchengerwa kwa kuwateua Wajumbe wa Bodi