December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Maryprisca atembelea gereza la Ruanda kuadhimisha Siku ya Wanawake

Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Mbeya

KATIKA kuadhimisha sikukuu ya wanawake duniani mbunge Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ametembelea Gereza la Ruanda Jijini Mbeya na kutoa msaada wa vitu mbali mbali ambavyo ni muhimu kwa wanawake.

Naibu waziri wa maji Mhandisi MaryPrisca Mahundi akimkabidhi msaada wa vitu mbalimbali mkuu wa sehemu ya wanawake Gereza la Ruanda Jijini Mbeya ,Rehema Mwailunga.

Aidha Mhandisi Mahundi ameahidi kutoa magodoro kumi(10) kwa ajili ya wanawake baada ya kupokea changamoto kutoka kwa wafungwa na mahabusu wanawake.

Hata hivyo mhandisi Mahundi amesema wanawake waliopo gerezani wapo ambao wamehukumiwa na wengine kesi zao bado zinaendelea kusikilizwa.

“Leo tumefika hapa kuwaona wanawake wenzetu na kuwafahamisha na huko nje yanayoendelea na tumewakumbuka, mpo huku kwa matatizo ya hapa na pale tukiamini kesho watarudi uraiani tokea wakiwa huku tukaona ni vema tuwatembelee na kuwapatia mahitaji muhimu kwa mwanamke ambayo ni lazima atumie”amesema Naibu waziri.

Akielezea zaidi Mhandisi Mahundi amesema kuwa amekuta changamoto ya ufinyu wa mabweni ya kulala ambapo askari wanawake wanaowatunza wafungwa wanawake walimweleza Naibu waziri.

Kwa upande wake Naibu spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Dkt.Tulia Akson amempongeza Naibu waziri wa maji kwa jitihada za kutembelea gereza la wanawake na kuwasaidia.

Kwa upande wake mkuu wa sehemu ya wanawake Gereza la Ruanda Jijini hapa,Rehema Mwailunga amesema kuwa suala la zima la urekebishaji wamesaidia kwani kuna wakati mwingine serikali inakuwa ngumu kutimiza.mahitaji yote kwa wakati.

Aidha amesema kuwa wafungwa wanawake wamefurahi kuona kwamba nao wanawajali na kuwa hiyo itasaidia suala zima la urekebishaji wa tabia.