December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Maryprisca akagua miradi ya maji Chunya

Na Esther Macha,TimesMajira Online,Mbeya

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi ,Maryprisca Mahundi ametembelea na kukagua miradi ya maji ya Makongolosi na Matundasi Wilayani Chunya mkoani Mbeya miradi hiyo inatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa maji wa Makongolosi unaotekelezwa kwa gharama ya sh.Bilioni 2.8 Naibu Waziri Mahundi amesema mradi huo utakamilika ndani ya wakati na kuwataka wananchi wasiwe na mashaka na nia ya dhati ya serikali kuhakikisha inamtua mama ndoo ya kichwani ya maji.

Aidha,amepongeza jitihada zinazofanywa na mkandarasi kampuni ya M/S Make Engineering & Water Work LTD JV Csmos Engineering Company pamoja na viongozi wa Sekta ya maji katika mkoa wa Mbeya.

Amesema mkandarasi huyo amekuwa makini na mwaminifu katika kuhakikisha miradi yote anayopewa inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango stahili.

“Niwaombe wakandarasi wengine waige mfano wa huyu mkandarasi najua mkandarasi anadai fedha shilingi milioni 270 namuahidi kuwa fedha zote zitalipwa ndani ya mwezi huu ili kazi ikamilike, wananchi wa Makongolosi wapate huduma ya maji.” Mhandisi Mahundi amesema.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa RUWASA wilaya ya Chunya ,Mhandisi Ismail Ismail amesema mradi wa maji wa Makongolosi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.8 ujenzi wake umefika asilimia 90.

Kwa upande wa mradi wa maji wa Matundasi unaotekelezwa kwa kutumia wataalam wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mahundi amesema ni moja ya miradi mizuri inayothibitisha ubora wa wasimamizi.

“Niendelee kuwapongeza na kuwatakia kazi njema Mnasimamia vizuri mradi unakwenda vizuri”amesema.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mahundi amekabidhi pikipiki kwa jumuiya ya watumia maji katika eneo la Matundasi kwa lengo la kurahisisha shughuli za usimamizi wa mradi wa maji katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo Mhandisi ,Tanda John amesema kuwa atahakikisha kazi iliyobaki inakamilika mapema iwezekanavyo.

Naye mkurugenzi wa mamlaka maji Safi na usafi wa mazingira Jijini Mbeya ,CPA Gilbert Kayange amesema kuwa watashirikiana na wakala wa maji vijijini (Ruwasa) katika kuwahudumia wananchi.

Naibu Waziri Mahundi ataendelea na ziara katika maeneo mbalimbali mkoani Mbeya ambapo atapata wasaa wa kuzungumza na wananchi .