Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Katika mwaka wa fedha wa 2022/23 Shirika la Nyumba la Taifa(NHC)limepanga kukusanya kiasi cha bilioni 268.03 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato.
Huku pia limepanga kuendelea na miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa mradi wa nyumba 1,000 za gharama nafuu Jijini Dodoma kwa ajili ya kuuza na kupangisha.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula katika mkutano na waandishi wa habari wa ufafanuzi juu utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2022/23 uliofanyika jijini Mwanza.
Dkt.Angeline ameeleza kuwa mbali na hayo pia shirika hilo litakamilisha ujenzi wa mradi wa Morocco square na kuendelea na miradi katika kiwanja Na. 711 Kawe, Golden Premier (GPR-Project na ujenzi wa nyumba 500 katika eneo la Kawe kwa ajili ya wananchi wa kipato cha kati cha chini.
Ambapo nyumba 360 zitajengwa awamu ya kwanza na nyumba 140 zitajengwa awamu
ya pili huku likifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa michoro katika miji ya
pembezoni (Satellite Cities) ya Kwala – Ruvu, Mbezi One Riffle Range (Dar es Salaam) na Kawe.
Ameeleza sanjari na hayo shirika litaendelea na ujenzi wa majengo ya biashara katika maeneo
mbalimbali nchini ikiwemo Bukoba, Mwanza, Dodoma, Kahama,Morogoro, Masasi na Lindi pamoja na kuandaa mpango kabambe wa matumizi ya ardhi katika maeneo ya Iwambi na Mwashiwawala – Mbeya, Uvumba – Dar es Salaam na Mafuru Village Morogoro.
Pia ameeleza kuwa litaendelea na utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ikiwemo ujenzi
wa majengo ya ofisi za Wizara nane (8) Jijini Dodoma, ujenzi wa jengo la shule ya uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,ujenzi wa majengo matano (5) ya Wakala wa Ununuzi wa Serikali(GPSA).
Ujenzi wa jengo la TANZANITE Mirerani, ujenzi wa Jengo la kitengo cha moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI) na miradi mingine itakayojitokeza.
Aidha ameeleza kuwa shirika litaendelea na usimamizi wa miradi mbalimbali ya kimkakati
ikiwemo soko la Kariakoo ambalo liliungua, kuendelea kutekeleza mpango wa miaka mitano wa ukarabati wa nyumba za shirika unaoishia mwaka 2027.
Pamoja na kununua ardhi ekari 400 katika maeneo mbalimbali ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na akiba ya ardhi na kuanza utekelezaji wa sera ya ubia itakayoruhusu sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa maeneo ya shirika.
Vile vile shirika hilo litaendelea na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi hususani kokoto na matofali,kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya nyumba na kulitangaza shirika na sekta ya miliki nchini kupitia vyombo vya habari.
“Shirika litashirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo,litaandaa eneo na baadae kujenga Sports Arena itakayochochea ukuaji wa mji wa kitovu cha mji wa Kawe,”ameeleza Dkt Angeline.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato