November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mabula atoakibano jijini Dar

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ametoa siku 14 kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam kukaa na kampuni za upimaji ardhi mkoani ili kuhakikisha urasimishaji unakamilika kwa wakati uliopangwa.Waziri Mabula aliyasema hayo kwenye viwanja vya Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumzia na wananchi.

Alizitaka kampuni hizo ambazo zimechukua fedha za wananchi na kushindwa kukamilisha kazi kurudisha fedha lakini pia kufutwa, ili iwe fundisho kwa makapuni mengine ambayo yanafanya kazi kinyume na taratibu.

Aidha Waziri Mabula alimtaka Mkurugenzi Manispaa ya Temeke pamoja na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Dar es Salaam kuhakikisha maombi yote ya hati ambayo wananchi wamewasilisha pamoja na kukamilisha malipo yawe yamefanyiwa kazi na wananchi wamepatiwa hati zao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Dkt. Mabura aliziagiza halmashauri zote nchini ambazo ni mamlaka za upangaji ardhi nchini kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya kupima, kupanga na kumilikisha ardhi badala ya suala hilo kubaki ni mzigo kwa Wizara wakati ni majukumu ya halmashauri kufanya kazi hiyo. Waziri Mabula pia alipiga marufuku Mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kutoa hati zinazozalishwa kwa njia ya analojia kwa wakazi wa Jiji hilo na badala yake watoe hati za kidijitali, kwani mfumo wa ILMIS unafanya kazi .

Aliwataka kuendelea kuhuisha kanzi data za ardhi katika mfumo wa kidijitali na kuzitaka halmashauri nyingine nchini kuendelea na zoezi hilo.

Aidha Dkt. Mabula alionya wale wote wanaoendelea na uvamizi katika maeneo ya watu bila kwenda ofisi za halmashauri nchini kujiridhisha kuwa wanatenda kosa la jinai na kuonya watendaji kata na vijiji kuacha kuuza ardhi kwani hilo sio jukumu lao bali wenye mamlaka hiyo ni Ofisi za Halmashauri.

Dkt. Mabula aliongeza kuwa wananchi lazima wafuate sheria za ardhi zilizopo na kuonya kuwa kuna baadhi ya watu waliofanya uvamizi na wakatakiwa kulipa mwenye eneo lake lakini wameshindwa kufanya hivyo kwa mantiki hiyo sheria zitafuatwa na kuhakikisha wanatolewa katika maeneo hayo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ndata Ludigija aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Temeke katika hotuba yake ya kumkaribisha mgeni rasmi ili aweze kushiriki zoezi la utoaji hati kwa wananchi hao alisema kuna watu wanapoteza umiliki kutokana na kutopima ardhi suala linalopelekea migogoro ya ardhi kwani kuna baadhi ya wananchi hapa Nchini wakijua eneo halina hati wanatengeneza Nyaraka feki na kupora mari za wananchi.