Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Sulaiman Jafo amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hashil Abdallah kuhakikisha anaweka mazingira bora ya kufanya biashara nchini Tanzania kwa kuondoa changamoto za kisheria na kikanuni zinazowakwamisha wafanyabiashara.
Amri yake kwa Katibu Mkuu wa Wizara ni kuhakikisha kuwa Changamoto za kisheria au kikanuni zinazowazuia wafanyabiashara kushiriki kikamilifu kwenye ushindani zitatuliwe, Utafiti wa kina ufanyike kubaini maeneo yote yenye vikwazo vya kisheria au taratibu zinazowakwamisha wafanyabiashara lakini pia Taarifa sahihi zipelekwe.
Waziri Jafo alitoa maagizo hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya ushindani yaliyofanyika jijini Dar es salaam yakienda sambamba na kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni “Sera ya ushindani na kudhibiti kukosekana kwa usawa katika uchumi”ambapo alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha mazingira ya ushindani kwa wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia sekta binafsi.
“Katibu mkuu wizara ya viwanda na biashara hakikisha kwamba tuangalie kama kuna changamoto ya kisheria yoyote ama kikanuni inayowakamisha wafanyabiashara wakashindwa kushiriki vizuri katika upande wa ushindani, hakikisha unawasilisha maeneo yote ya kisheria ambayo huwenda yanachangamoto ya kisheria kwa wafanya biashara”
Aidha Waziri Jafo amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio kuhakikisha wanaimarisha mifumo ya kibiashara nchini na michakato yote ya mapitio ya maunganiko ya kampuni wanayafanya kwa haraka lengo ni kusaidia vijana wa kitanzania wapata ajira
“Vijana wengi wanamaliza vyuo vikuu na serikali haiwezi kuajiri wote hivyo FCC lazima tutengeneze mazingira ya haraka yale makampuni ambayo yanataka kuongeza uzalishaji hasa katika miunganiko ya makampuni haya endeleeni kwa haraka lengo ni kwamba tunahakikisha tunachagiza uwekezaji”
Kadhalika Waziri Jafo alisisitiza juu ya umuhimu wa watumishi wa serikali kuchangia katika kuharakisha uwekezaji nchini ambapo alihimiza watumishi kutumia juhudi na maarifa yao kuhakikisha kwamba kila fursa ya uwekezaji inatimizwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Aliongeza kwa kuyataka makampuni kuhakikisha wanashindana kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji bila kufanya udanganyifu wa aina yoyote ili kuweza kupata masoko ya ndani na nje na hivyo kukuza uchumi wa nchi .
Waziri Jafo aliwataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali na wa wanapozipata wafanye kazi kwa juhudi, maarifa na uaminifu .
“Katika upande wa viwanda wanatamani kupata vijana ambao waaminifu imani yangu kubwa kutokana na utamaduni wetu watanzania wale watakaopata fursa hakikisheni tunatumia fursa vizuri kuhakikisha tunaweza uaminifu kwa nchi yetu”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa tume ya FCC Dkt Aggrey Mlimuka alisema kuwa tume hiyo inawajibu na kusimamia uwepo wa fursa sawa kwa washindani wakubwa na wadogo katika soko, na kupunguza ukiritimba katika masoko kwa kuhakikisha washindani wakubwa hawawazuii washindani wadogo kukua na kuingia au kuwatoa sokoni.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Wiliam Erio alisema hayo ni maadhimisho ya kwanza ya siku ya ushindani duniani tangu kufanyika marekebisho ya sheria nchini.
“Tunamshukuru sana Rais samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge kwa kufanikisha kupitisha kwa marekebisho na kuwa sheria jambo ambalo litatuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam