January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Gwajima: Madiwani Dar es Salaam mmewapa mtihani madiwani wengine vita dhidi ya Ukatili.

Na Mwandishi wetu, Timesmajira online

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima amesema kitendo cha Madiwani Wanawake wa Mkoa wa Dar Es Salaam kujitokeza na kuanza Kampeni ya kutokomeza ukatili ndani ya jamii ni chachu kwa wengine nchini, kwani Vita ya Ukatili bila Viongozi kuungana na Wanajamii kupigana itakuwa vigumu kuvishinda.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo, Julai 23, 2022 alipokuwa akifungua Kongamano la Madiwani wanawake kwa mkoa huo ambapo pamoja na mambo mengine Madiwani hao wamekabidhi Hundi ya zaidi ya milioni tano kwa hisani ya Benki ya NMB kwa ajili ya kuwawezesha kupata vitambulisho vya Bima ya Afya watoto 100 waishio kwenye mazingira magumu katika awamu ya kwanza.\

“Ninyi Madiwani Wanawake wa Mkoa huu mmeonesha njia, huu ni wito kwa viongozi wengine nchini kwamba nao wainuke na kupaza sauti zao dhidi ya Ukatili unaoendelea ndani ya Jamii” alisema Waziri Dkt Gwajima.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha tatizo la unyanyasaji na ukatili wa Kijinsia linatokomezwa hapa nchini. Hii ni kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 Ibara ya 231 (k) na (l) inayoelekeza bayana umuhimu wa kuimarisha huduma za msaada wa Kisheria katika huduma za jamii.

Aidha kuhusu hali ya takwimu za Ukatili Dkt. Gwajima alisema katika kipindi cha mwaka 2020 na 2021 Jeshi la Polisi limeripoti jumla watoto 27,369 wakifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali (sawa na wastani wa 1140 kila mwezi), ilihali kwa mwaka 2021 waliobakwa walikuwa 5899 sawa na wastani wa 491 kwa mwezi na waliolawitiwa ni 1114 sawa na wastani wa 93 kwa mwezi. Kwa upande mwingine, haya hayo yote hutokea nyumbani kwa 60% na shuleni 40%.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Madiwani Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Rehema Ayubu amepongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunda Wizara hiyo na kumteua Dkt. Gwajima kuingoza kwani no Wizara muhimu katika kuhudumia Jamii hasa kupambana na vitendo vya ukatili.

“Mhe. Waziri sisi Madiwani Wanawake wa Mkoa huu, tunaona na kushuhudia hatua mbalimbali unazochukua wewe na wasaidizi wako ndani ya wizara dhidi ya madhila haya ya ukatili ndani ya Jamii, tunakuahidi ushirikiano wetu kwani kwa nguvu moja tutashinda” alisema Mhe. Rehema.

Naye Katibu Mkuu, wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Dkt Zainab Chaula alisema yeye kama Mtendaji Mkuu anaamini katika matokeo hivyo wanapoona wadau mbalimbali wanaunga mkono jitihada za kutokomeza ukatili wanapata faraja kuwa wadau na Jamii wanaunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na vitendo hivyo.

Dkt. Gwajima ameendelea kupokea na kukutana na wadau mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuweka mbinu za pamoja kwa kushirikiana na Kampeni Huru ya Jamii ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa nchini “SMAUJATA” ili kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili ndani ya jamii.