Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Dodoma
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk.Dorothy Gwajima amelitaka Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kuitisha uchaguzi kwa wakati badala ya kutegemea tena Waziri kuingilia mchakato huo.
Dkt.Gwajima amesema hayo jijini hapa leo wakati akizindua baraza hilo jipya baada ya kufanya uchaguzi na kupata viongozi wapya.
“Tusiruhusu watu wachache kuirudisha NacoNgo kule ilikotoka na kuligeuza Baraza kuwa kitega uchumi,”amesema.
Vilevile amelitaka Baraza hilo jipya kufanyakazi kwa weledi,uadilifu na uzalendo na hali ya juu kwa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali na Taifa kwa ujumla na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria ,kanuni na miongozo iliyopo ili kukidhi matarajio ya waliowachagua na jamii ya watanzania kwa ujumla.
Akijibu mapendekezo yaliyotolewa na ya iliyokuwa kamati ya mpito ya uchaguzi wa Baraza hilo,Dkt.Gwajima amesema yanahitaji kujitoa kwa baraza hilo pamoja na wizara yake.
“Masuala ya uwakilishi wa kikanda,afua za utekekelezaji,uelewa wa wadau kuhusu Baraza na mapito ya kanuni za uchaguzi wa baraza ni masuala mnayoweza kuyajadili kupitia mifumo yenu ya ndani na kuchukua hatua kwa kuzingatia sheria na kanuni.
“Masuala ya mafunzo kwa wasajili wasaidizi kuhusu masuala ya uchaguzi,pamoja na mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wapya wa Baraza yapo ndani ya wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali na niwahakikushie kuwa tayari tulianza mchakato wa kutoa mafunzo kwa wasajili wasaidizi na zoezi hilo ni endelevu,”amesema.
Aidha, amesema suala la kuwajengea uwezo wajumbe wapya na baraza lipo na ndani ya uwezo wa wizara yake na milango ipo wazi wakati wowote.
“Tuna wataalam wa kutosha kwenye masuala ya sheria, uratibu na tayari nimesikia tayari mmeshaanza kidogo kupata semina elekezi kuhusu sheria na kanuni,uratibu wa mashirika na msingi wa ushirikiano baina ya serikali na sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali,”amesema.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua