Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara
SERIKALI imeyataka Mashirika ya Kiraia yanayojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia pamoja na Wadau wote kwa ujumla,kuelekeza nguvu nyingi za utoaji wa elimu ya ukatili Vijijini ambako bado vitendo hivyo vinafanyika kwa kiwango kikubwa tofauti na maeneo ya mijini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dkt.Dorothy Gwajima ameyasema hayo Disemba 9, 2024, katika kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia Kitaifa yaliyofanyika Uwanja wa shule ya Sekondari Ingwe Nyamongo Wilayani Tarime Mkoani Mara.
Ambapo wadau mbalimbali kutoka Serikalini, Mashirika ya Kiraia, Taasisi za Dini, Wazee wa Kimila, na Wananchi wameshiriki katika kilele hicho chini ya kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “kuelekea miaka 30 ya Beijing chagua kutokomeza ukatili wa Kijinsia”
Waziri Gwajima amesema kuwa, kukosekana kwa kiwango kikubwa Cha elimu maeneo ya Vijijini kumeendelea kuchangia kushamiri kwa matukio mbalimbali ya ukatili ambayo pia wakati mwingine hayaripotiwi katika vyombo vya sheria licha ya madhara yake kuwa makubwa kwa wanaofanyiwa.
Amesema, Wananchi wa mijini wamekuwa wakifikiwa na elimu hiyo kwa kiwango kikibwa kwa njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya Habari hivyo basi Kasi hiyo pia ipelekwe pia Vijijini ili kuleta mabadiliko chanya kwa Wananchi wa maeneo yote ya mijini na Vijijini.
Pia, Dokt.Gwajima amesema mkoa wa Mara umeendelea kupiga hatua katika kutokomeza vitendo vya Ukatili wa Kijinsia ukiwemo ukeketaji ambao umeshuka hadi asilimia 28, na kutoka nafasi ya kwanza kama ulivyokuwa hapo awali. Na mikoa ya Arusha na Manyara ikiitaja kuongoza hapa nchini ambapo ina fungana ikiwa na asilimia 43.
“Ukeketaji Mara umeendelea kupungua kwa mujibu wa Tafiti za kitaifa za Idadi ya Watu na Afya Tanzania za mwaka 2022. Mkoa wa Mara una asilimia 28, na kiwango cha ukeketaji kitaifa umepungua kwa asilimia 2, Mkoa wa Arusha una asilimia 43, Manyara asilimia 43, Singida asilimia 20, Tanga asilimia 19, na Dodoma asilimia 18.” amesema Waziri Dkt. Gwajima na kuongeza.
“Mambo ya ukatili, Tuanze kuiondoa Mara kwenye sura ya ukatili wameshaitikia, elewa pasi na shaka kwa sababu ya Viongozi wenu wakuu wote wanashirikiana pamoja na Jamii na Wazee wetu wa kimila.”amesema Dkt.Gwajima.
Aidha amewashukuru Wazee wa Kimila kutoka Koo 12 za kabila la kikurya kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kupiga vita vitendo vya ukeketaji na amewahimiza kuzidi kutoa elimu katika Jamii akisema madhara ya ukatili yanarudisha nyuma juhudi na jitihada za maendeleo na kuhatarisha afya na usalama wa wanawake hasa wanaokumbana na ukeketaji,vipigo ndoa za utotoni na ukatili mwingine.Â
Kwa upande wake Mark Njera Ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara amesema kuwa “Msimu huu ni wa ukeketaji, Koo tisa Kati ya Koo 12 zinakeketa.Kwa kutambua jambo hilo kipindi hiki cha siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia elimu imetolewa na Maofisa wa Polisi Dawati la Jinsia na Watoto wapatao 150 kutoka Mikoa yote ya Tanzania hapa Tarime ambapo walianza kutoa elimu hiyo kuanzia Dicemba 3, 2024, hadi Decemba 9, 2024.”amesema na kuongeza kuwa.
“Elimu imetolewa kwa wanafunzi wa shule za Msingi wapatao 13,000, wanafunzi wa shule za Sekondari 11,000, kata 48, minada, makanisa na vikundi. Na katika kipindi hicho Wasichana 113, wameokolewa katika hatari ya kukeketwa, tunaomba serikali iweze kutunga sheria ya kushughulikia ukeketaji.”amesema Kamanda Njera.
Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara amesema ili kumaliza tatizo la ukeketaji ni vyema elimu inayotolewa iwe shirikishi kutokana na jambo hilo kuwa ni la kimila na pia mfumo dume bado upo. Huku akikiri ukatili kwa sasa umepungua kwani awali matukio mengi ya ukatili yalishamiri sana na wakati mwingine yalifanywa hadharani.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais