Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikitishwa na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za Manispaa na Wilaya ya Iringa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kusababisha halamshauri hizo kushindwa kukusanya maduhuli ya serikali yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.
Akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Iringa Novemba 30, 2022 kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi, Dkt. Mabula alibaini uzembe wa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi wakiwemo maafisa ardhi wateule kwa kushindwa kusimamia utoaji hati za ardhi na uingizaji milki za ardhi kwenye Mfumo wa Utunzaji Kumbukumbu za Ardhi kwa njia ya kielektroniki.
Amewataka maafisa ardhi wateule katika halmashauri hizo kujitathmini kutokana na kushindwa kwao kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha wananchi wanamilikishwa na kupatiwa hatimiliki za ardhi.
Aidha, Waziri wa Ardhi Dkt Mabula amewataka maafisa hao wa sekta ya ardhi katika halmashauri hizo mbili za mkoa wa Iringa kuhakikisha kufikia Desemba mwaka huu wa 2022 wawe wamewasilisha taarifa zao za makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na hatua walizochukua kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.
“Maana hata idadi ya viwanja mlivyonavyo hamvijui hilo ni kosa, unawezaje kukaa bila kujua idadi ya viwanja vyako katika halmashauri yako. Nataka kabla sijaondoka hapa nijue idadi ya viwanja mlivyokuwa navyo ni vingapi, na vingapi vipo kwenye mfumo na kwa nini havijaingia kwenye mfumo kwa hundred percent” alisema Dkt Mabula.
Aliongeza kwa kusema kuwa, mtendaji wa sekta ya ardhi hajui idadi ya viwanja vilivyopo kwenye mfumo wa utunzaji kumbukumbu za ardhi anawezaje kudai madeni? na kubainisha kuwa wamiliki wa ardhi wanapotambulika kwenye mfumo inakuwa ni rahisi kwa watendaji kudai madeni.
“Huna idadi maalum ya viwanja na hujaingiza kwenye mfumo wa utunzaji kumbukumbu unawezaje kudai madeni? Alihoji Dkt Mabula
Amewataka wakurugenzi wa halmashauri katika mkoa wa Iringa kutimiza wajibu wao wa kuzisimamia sekta za ardhi kwenye halmashauri zao kwa kuwa idara za ardhi ni za kwao na si za wizara na kubainisha kuwa watendaji wa sekta ya ardhi ni chachu ya kutoa elimu katika masuala ya ardhi.
Katika ziara yake Dkt Mabula amekutana na watumishi wa sekta ya ardhi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Iringa pamoja na wale wa halmashauri ya Manispaa na  Wilaya ya Iringa lengo likiwa kuboresha utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Mkoa wa Iringa unazo jumla ya halmashauri tano ambazo ni Manispaa ya Iringa, Mafinga Mji, Irinda DC, Kilolo DC na Mufindi DC.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini