December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Mabula aipa wiki mbili Halmashauri ya Serengeti

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameipa wiki mbili halmashauri ya wilaya ya Serengeti mkoani Mara kumpatia taarifa ya hali ya mashamba 36 yaliyopo katika halmashauri hiyo ili yale mashamba yasiyoendelezwa yaweze kubatilishwa umiliki wake.

Hatua hiyo inafuatia kuelezwa kupitia taarifa ya sekta ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Serengeti kuwa wilaya hiyo ina mashamba yaliyopimwa 36 kulingana na taarifa iliyopatikana kutoka wizarani kutokana na kutokuwepo kumbukumbu za kutosha mashamba hayo katika wilaya hiyo.

Taarifa hiyo iliyosomwa na Afisa Ardhi Mteule wa Halmasahauri hiyo ya Serengeti Orwaka Nyamsusa ilieleza kuwa, mashamba hayo yalipimwa vijijini bila kufuata taratibu za uhaulishaji na ilipotakiwa yamililishwe kwa kupewa hati za kawaida ilishindikana.

“Ninawapa Serengeti wiki mbili nijue status ya mashamba hayo na kama ni suala la kuanza kuyabatilisha, mchakato uanzie katika halmashauri ambayo ni mamlaka ya upangaji ili tuitangaze fursa kwa wawekezaji kama Serengeti tunayo mashamba 36 na kati ya hayo ni matano tu yenye umiliki halali’’. Alisema Dkt Mabula