Fresha Kinasa ,Times MajiraOnline.
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wanaume wawe jawabu katika Jamii la kumaliza tatizo la ukatili wa Kijinsia ukiwemo ukeketaji ili kujenga jamii yenye ustawi bora.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo Februari 12, 2026 Katika Kilele cha maadhimisho ya kutokomeza ukeketaji, ambapo kitaifa imefanyika Katika Kijiji cha Losirwa Kata ya Esilalei Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.
Ambapo, Viongozi wa Serikali na Wadau wa mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na Wananchi wamehudhuria. Huku kauli mbiu kwa mwaka huu ikisema, “Sauti yetu, tokomeza ukeketaji”

Katika hotuba yake Waziri Dkt. Gwajima amesema, ukeketaji bado upo na juhudi za pamoja zinahitajika kuweza kuutokomeza, huku mikoa ya Arusha na Manyara akiitaja kuongoza kwa asilimia 43, Mara asilimia 28, Singida asilimia 20, Tanga asilimia 19, Dodoma asilimia 18, Iringa asilimia 12, Morogoro asiliamia 10, na Pwani asilimia 5.
Amesema wanaume wanatakiwa watumie Mamlaka yao kujenga ushawishi wa kukemea ukeketaji kwani unapaswa kukomeshwa. Huku akisema, ukeketaji ni kosa kisheria, na Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wote wanaobainika kufanya hivyo.
“Wanaume kama tumeamua kuupinga ukeketaji naomba tusaidiane kuleta majawabu. Wanaume nahitaji msimame kidete kupinga ukeketaji kwa juhudi zote, Kuoa mwanamke aliyekeketwa mkisema haiwezekani hili linawezekana kabisa. Vita hii kuishinda kwa Wanawake peke yao haiwezekani Wanaume mnahitajika kulimaliza jambo hili kwa pamoja.”amesema Dkt. Gwajima.
Pia Dkt. Gwajima ameitaka Jamii kuweka mkazo katika kuwasomesha Watoto wa kike kwa ufanisi kwani wanayo fursa kubwa ya kuendelea kuleta mageuzi chanya ya kimaendeleo katika Jamii na kuachana na kasumba ya kuwaoza katika umri mdogo kwa ajili ya kupata fedha.
“Wewe Ngariba unayetaka mtaji wa biashara kwa kukeketa, utafungwa, ni vyema utumie fursa za kibiashara. Serikali inatoa fursa nyingi kiuchumi ikiwemo mikopo, tumieni mikopo hiyo badala ya kutegemea kipato kidogo unacholipwa kwa kumkeketa mtoto wa kike.” amesema Dkt. Gwajima.
Frank Kiwango ni Dkt. Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili ambapo amesema ukeketaji una madhara ikiwemo Sonona, hofu iliyopitiliza, kiwewe, kukosa uhuru wa mwili, hatari ya Magonjwa ya kuambukiza na hisia ya usaliti.

Laiza mosha ni mkazi wa Losirwa amesema kuwa, wanaume wakishiriki kikamilifu katika kupambana na ukeketaji utaisha. kwani mipango mingi ya ukeketaji hupangwa na wao na ndio Kichwa ya familia.
Katika Kilele hicho, Waziri Dkt. Gwajima amezindua Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa kutokomeza ukeketaji wa mwaka 2025/26 – 2029/30. Ambapo una malengo makuu manne ikiwemo kufanya jamii kukataa ukeketaji, kuimarisha mfumo wa utoaji huduma kwa waathirika, kuimarisha uratibu na kufanya utafiti.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama