January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Chana akabidhi madawati 90 shule ya msingi Manga

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Mhe. Balozi,Dkt. Pindi Chana amekabidhi madawati 90 yenye thamani ya shilingi milioni 7 kwa Shule ya Msingi Manga iliyopo katika Kijiji cha Manga, Wilayani Ludewa Mkoani Njombe leo Septemba 17, 2024.

Madawati hayo yametolewa kwa udhamini wa Benki ya CRDB ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za elimu bure pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Elimu.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya madawati hayo, Mhe. Chana amesema kufuatia jitihada hizo za benki ya CRDB ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha mtoto wake anaenda shule.

“Elimu ni suala la msingi sana Serikali ya Dkt. Samia itaendelea kuwekeza katika Sekta ya Elimu kwa kuhakikisha tunatoa madarasa na vitendea kazi vya uhakika ili kila mtoto apate elimu bora” amesisitiza.

Aidha,ametumia fursa hiyo kuishukuru benki ya CRDB kwa madawati hayo.

Naye, Meneja wa Benki ya CRDB, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jenipher Tondi amesema kuwa benki ya CRDB kila mwaka imekuwa ikitenga asilimia moja ya faida yake kwa ajili ya kusaidia miradi ya kijamii kama elimu, mazingira, afya, uwezeshaji wa vijana na wanawake wajasiriamali na ndio maana ilipopewa ombi la kuchangia madawati haikusita.

Amesema madawati hayo yatasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Manga.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, wananchi, wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Manga.