January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Chana afurahishwa na hatua za ujenzi wa Nyumba za Wanangorongoro, asisitiza kazi Iendelee

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Tanga

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefurahishwa na kasi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambao wako tayari kuhamia kwenye makazi mapya yanayojengwa Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.

Mhe. Chana amefurahishwa na hatua ya ujenzi huo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na miundombinu ya huduma za kijamii kwa ajili ya wakazi wa Ngorongoro wanaotaka kuhama kwa hiyari ili kupisha shughuli za uhifadhi ndani ya eneo la Ngorongoro.

“Kwa sasa Ngorongoro idadi ya watu imeongezeka sana, Serikali imeamua kuwajengea mazingira bora ya kimaisha nje ya Hifadhi, katika Kijiji hiki tumewajengea nyumba za kisasa, miundombinu ya barabara, shule, hospitali pamoja na huduma ya maji ili wale watakaohamia eneo hili kwa hiyari yao waishi maisha mazuri kama watanzania wengine” alifafanua Mhe. Chana.

Katika ziara hiyo Mhe Waziri amekagua nyumba zaidi ya 100 zinazojegwa na Serikali kupitia wataalam wa NCAA na kuongeza kuwa sambamba na ujenzi wa nyumba hizo, Serikali imepanga kuongeza vyumba vya madarasa 10 vya shule ya sekondari na vyumba sita vya shule ya msingi vitakavyokidhi ongezeko la wanafunzi watakaohamia eneo hilo.

Aidha, msimamizi wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo hilo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Mhandisi Joshua Mwankunda amemueleza Mhe. Waziri kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 103 upo katika hatua nzuri za umaliziaji ambao pia unaambatana na uchimbaji wa visima vya maji, vyoo na kuchonga mtandao wa barabara unaozunguka makazi katika Kijiji hicho.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Adam Malima ameelezea kuwa, kila mtanzania anajua umuhimu wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kama eneo muhimu la urithi wa dunia na Watanzania wote wanapaswa kuilinda na kuinusuru hifadhi hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Amewahakikishia wananchi watakaohama kwa hiyari ndani ya hifadhi hiyo kuwa watapata sehemu nzuri na salama ya kuishi wao na mifugo yao na Uongozi wa Mkoa wa Tanga kupitia kamati ya Ulinzi na usalama unaandaa mazingira mazuri kuhakikisha wakati wowote Wananchi watakapohamia Kijiji cha Msomera wanakuwa salama na kupata huduma zote muhimu za kibinadamu.

Ameongeza kuwa Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine wapo kwenye hatua za kuhakikisha huduma za nishati, maji, elimu, afya, mawasiliano na barabara zinaimarishwa katika Kijiji hicho kinachopakana na vijiji vingine vya Mzeri, Kibaya, Wagi na Misima.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera Martin Oleikayo Paraketi amaesema wananchi wanaozunguka eneo la mradi wa Kijiji hicho wapo tayari kushirikiana na Serikali kuwakaribisha wananchi wanaohamia katika kijiji hicho na kuishukuru Serikali kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali.