Na Nuru Mwasampeta, WM
IMEELEZWA kwamba uwepo wa masoko ya madini, miundombinu ya barabara inayounganisha Tanzania na nchi nyingine jirani, uwepo wa bandari kubwa, uwepo wa viwanja vya ndege na ndege kubwa nchini, amani na usalama vinavyotawala nchini Tanzania ni vivutio tosha kwa wawekezaji wa sekta ya madini nchini.
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyasema hayo Mei 31, 2021 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliofika ofisini kwake kwa ajili ya kufanya naye mahojiano.
Akizungumza na waandishi hao wa habari, Waziri Biteko ameeleza kuwa, wizara yake imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha lengo la kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 650 iliyojipangia kwa mwaka 2021/2022 kinafikiwa kutokana na mikakati mizuri waliyojiwekea katika kuongeza makusanyo ya maduhuli ya serikali.
Amesema, mwaka wa fedha unaoisha, wizara ilipangiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 526 ambapo mpaka anapozungumza tayari imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 527 ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2020/2021 sawa na asilimia 109.3 ya lengo walilowekewa kukusanya.
Akizungumzia mikakati iliyowekwa na wizara ili kufikia malengo ya kukusanya kiasi hicho cha fedha, Biteko alisema mkakati wa kwanza ni suala la uongezaji thamani madini.
Biteko amesema, ili madini yanayochimbwa nchini yaweze kuongeza tija ni lazima suala la uongezaji thamani madini lipewe msukumo mkubwa.
“Tulikotoka ni mbali sisi kama nchi tulikuwa kiini au chanzo cha rasilimali ghafi kwa ajili ya viwanda vya wenzetu, tumehama huko sasa tunataka madini yaongezwe thamani hapa hapa nchini ili manufaa yaweze kuonekana,”amesema.
Katika kuhakikisha dhana ya uongezaji thamani madini inafikiwa, wizara imetoa leseni kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ambapo imejenga kiwanda kikubwa cha kusafisha dhahabu kwa kiwango cha kimataifa jijini Mwanza chenye uwezo wa kusafisha dhahabu yote inayopatikana nchini.
Ameongeza kuwa, kiwanda kingine cha kusafisha madini ya dhahabu (refinery) kimejengwa na mwekezaji mzawa na mmiliki wa kampuni inayoitwa Geita Gold Refinery mkoani Geita.
Pamoja na uwepo wa viwanda hivyo kiwanda kingine cha kusafisha dhahabu ni cha Eyes of Africa kilichopo mkoani Dodoma.
Aidha, Biteko amebainisha kuwa, wizara imetoa leseni nyingine tano kwa ajili ya ujenzi wa smelters ili kuongeza thamani madini aina ya tin,shaba, nickel huko Kyerwa mkoani Kagera ambapo mpaka sasa kuna smelters nne na Mpwapwa kuna smelter moja lakini pia leseni imetolewa kwa ajili ya ujenzi wa smelter mkoa wa kimadini wa Kahama.
Akizungumzia suala la madini ya vito, Biteko alisema Serikali imeondoa kodi mbalimbali ya vifaa vya kukatia madini (lapidaries) ili wachimbaji na wafanyabiashara waweze kukata madini hapa nchini.
Amebainisha kuwa, punguzo hilo la kodi limepelekea ongezeko la vifaa vya kukatia madini ambapo mpaka sasa kuna mashine 467 za kukatia madini na kuongeza thamani ya madini hayo.
Akizungumzia suala la utoroshaji wa madini, Biteko amesema, suala la ulinzi wa rasilimali madini si kazi ya wizara pekee na kuwataka watanzania wote kuwa na wivu na rasilimali zilizopo kwa kuwabaini wanaojihusisha na suala la utoroshaji wa madini ili kuhakikisha tabia ya kutorosha madini inakwisha.
“Yeyote anayedhani anaweza kutorosha madini akabaki salama kwenye nchi yetu, hana nafasi kwa sasa, nirudie kuwaambia yeyote anayetorosha madini anatafuta vitu viwili, anatafuta jela na umaskini na sisi tusingependa kuwaona watanzania wanakwenda jela kwa sababu ya kutorosha madini,”amesisitiza.
Akihitimisha mazungumzo yake na wanahabari, Waziri Biteko alitoa wito kwa wafanyabiashara wa madini kuja kununua na kuuza madini kwenye masoko yaliopo kila mkoa nchini.
Aidha, aliwaalika watanzania wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini nje ya nchi kuleta madini wanayoyachimba ili yaongezwe thamani kwenye viwanda vilivyojengwa kwa kazi hiyo nchini.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best