Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuifungua nchi kwa kuweka mazingira wezeshi na kuvutia uwekezaji na biashara kwa nchi zingine kwa kuimarisha ushirikiano na upatikanaji wa masoko kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Umoja wa Soko la Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa leo Oktoba 03, 2024 wakati akifungua mkutano wa mashirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Japani Ili kutekeleza miradi ya miundombinu na kuwekeza kwenye viwanda vya bidhaa za ujenzi.
“Mkutano wa leo kati ya Tanzania na Japan ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua nchi katika uchumi unaokua”
“Rais amefungua nchi ni kwamba nchi rafiki duniani sasa zinakuja tanzania kuangalia ni namna gani tutakua tunamashurikiano ambayo yatasaidia maendeleo ya Tanzania lakini pia wao kupitia nchi yetu waweze kupata masoko ya jumuhiya ya Afrika Mashariki”
Kutokana na hivyo Waziri Bashungwa amewataka Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji mbalimbali wanaofika nchini kuwekeza, kufanya biashara na kuondoa urasimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
“Tunamshukuru rais kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi na kuvutia uwekezaji ivyo watanzania tuendelee kuunga mkono wa jitihada hizo, mambo ya urasimu hayana nafasi kwa upande wa watumishi wa umma”
Kadhalika Waziri Bashungwa amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na Japani hususan katika Sekta ya miundombinu ambapo Tanzania inaendelea na mazungumzo na nchi hiyo ya kushirikiana katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kupunguza msongamano wa magari katika miji na majiji.
Ameeleza kuwa Tanzania imeanza mazungumzo na Japani ya kushirikiana katika usanifu na ujenzi wa barabara ya juu (FlyOver) katika eneo la Moroco jijini Dar es Salaam itakayopunguza msongamano wa magari na kurahisisha shughuli za kiuchumi.
“Sasa hivi tunaendelea na mazungumzo na Japani kuhusu ujenzi wa Flyover ya Moroco kwa kufanya usanifu na ujenzi pamoja na kuboresha maeneo mengine yenye mapishano ya barabara ili kupunguza matumizi ya taa za barabarani”, amesisitiza Bashungwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameeleza kuwa maendeleo ya nchi yoyote yanategemea sana sekta ya usafiri kwani ni kiungo muhimu kwa biashara ya ndani na ya kimataifa ambapo kwa sasa Tanzania ina jukumu muhimu kama lango la kimataifa kwa baadhi ya nchi jirani ili kurahisisha usafirishaji na upatikanaji wa soko la kimataifa.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda ameeleza umuhimu wa mkutano huo ambao umewakutanisha wabobezi katika ujenzi wa miundombinu bora na ya kudumu inayoweza kuhimili majanga kama vile matetemeko ya ardhi na vimbunga kutoka nchi ya Japan na hivyo watasaidia kutoa michango na uzoefu kwa makampuni ya ujenzi kwa nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania katika ujenzi wa miundombinu yote nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri amesema ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Japani umejikita zaidi kwenye sekta ya ujenzi,miundombinu , sekta ya uvuvi, na kilimo
Teri amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi na kuvutia uwekezaji nchini.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang