November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashungwa atoa onyo kali kwa wasanii

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa, ametoa onyo kali kwa wasanii ambao wanapeana maneno yasiyofaa mitandaoni kuacha mara moja kwani hatua kali zitachukuliwa juu yao .

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam leo, Bashungwa amesema wasanii wote kote nchini wajenge umoja na mshikamano na kuacha tabia za kitoto ili kazi ziweze kuendelea.

“Nitumie nafasi hii kuwaambia wasanii wetu kote nchini wajenge umoja na mshikamano, hayo yanayoendelea mtandaoni ya kitoto waondokane nayo kwasababu serikali tumedhamiria kuhakikisha wasanii wetu na wale ambao wapo tayari kushirikiana na serikali ili waweze kwenda mbele, tunataka wanufaike na sanaa yao na wengine wanufaike ambao wamewaajiri,” amesema Bashungwa.

Aidha amesema, wasanii wote waendelee kuzingatia maadili na tamaduni za kiafrika, kwasababu mambo yanayoendelea mitandaoni yanamchefua.

Pia Bashungwa ameongeza kuwa tasnia ya sanaa ina fursa kubwa ya kupelekea waliomo kwenye sanaa kuweza kunufaika hivyo wanatumia njia iwezekanayo kuwasaidia wasanii kwa weledi mkubwa.

“Sanaa, ni tasnia ambayo ina fursa kubwa ya kusaidia waliomo kwenye tasnia hii wanufaike zaidi na kuweza kutengeneza ajira nyingi hivyo nimeomba wahisani wa maendeleo tukutane na tujadiliane, vipaumbele ambavyo tumeshavitengeneza ndani ya serikali kutoka kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 kile ambacho serikali tumekipanga tuangalie ni namna gani wahisani wataongezea ili tuweze kuwasaidia wasanii wetu kwa weledi mkubwa zaidi,” amesema.

Waziri Bashungwa amesema, Kwenye bajeti wanayoipeleka bungeni mfuko wa maendeleo wa sanaa na utamaduni wamepanga kutenga bilioni 1.5 lakini mpaka itakapopitishwa bungeni na anaamini bajeti hiyo itapita vizuri.

%%%%%%%%%%%%%%%%%%%%