September 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashe aingilia kati sakata la ufyekaji mahindi Mpanda

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Mpanda.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amehimiza watendaji wa umma kuongoza kwa utu na busara kwa kuwa wanaongoza raia ambao kipato chao ni kidogo na ardhi walizonazo ni hizo kwenye makazi yao.

Hayo yamesemwa baada kutokea ukataji wa mashamba ya mahindi yanayokadiriwa kufikia hekari zaidi ya sita Desemba 13 mwaka huu katika eneo la Mpanda Hotel Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi kwa kile kinachotajwa na baadhi ya maofisa wa Manispaa hiyo kuwa kuendesha kilimo cha mazao marefu katika maeneo ya mjini ni kinyume cha sheria.

Waziri huyo akinukuliwa kupitia mtandao wa X akisikitishwa na kitendo hicho kilichofanywa na watu wanaodhaniwa kuwa ni Jeshi la Akiba (Migambo) kwa madai ya kutekeleza maagizo kutoka uongozi wa Manispaa hiyo.

Bashe amesema kuwa sheria inawapa haki wananchi kufanya kilimo maeneo ya pembezoni na makazi yao.

”Salaam ndugu zangu nimeongea na Meya wa Manispaa ya Mpanda kumuomba wasimamishe operation wanavyofanya kukata mashamba ya mahindi yaliyolimwa pembezoni mwa kaya za wananchi wa Manispaa hiyo,” ameandika Waziri wa Kilimo Bashe.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko akiandika kupitia moja ya mtandao wa kijamii amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Mpanda kusimamia maelekezo yake ya kutokukata mazao yaliyolimwa mjini Mpanda.

” Katika kipindi hiki cha mpito Manispaa ifafanue sheria na taratibu za Manispaa,ikiwemo kilimo mijini kwa wananchi wote ili waelewe na kutekeleza ili kuepuka sintofahamu kama hii iliyotokea Kata ya Mpanda Hotel,” ameandika Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

Aidha, Mrindoko ametoa pole kwa waathirika pamoja na kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Katavi kuendelea kuchapa kazi huku wakizingatia sheria mbalimbali zilizowekwa na mamlaka.

Naye Msitahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi, Haidary Sumury amekiri kupigiwa simu na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akitaka kupewa ufafanuzi wa taarifa za ukataji wa mashamba ya mahindi.

Sumury amesema kuwa alipokea maagizo ya Waziri huyo na zoezi la ukataji wa mashamba ya mahindi umesitishwa tangu Desemba,16 mwaka huu katika maeneo hayo.