Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Masasi
ILI kuhakikisha mazingira ya elimu yanaboreshwa na kuongeza ufaulu wa wanafunzi wilayani Masasi mkoani Mtwara, Mbunge wa Masasi ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Godffrey Mwambe amekabidhi magari matatu kwa shule tatu za sekondari wilayani hapa.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi magari hayo, Mbunge huyo amesema amekabidhi magari hayo yakiwa sehemu ya mpango na mkakati Serikali ya Awamu ya Sita wa kuboresha mazingira ya elimu nchini na kuinua ufaulu.
“Leo ninakabidhi magari haya kwenu yaende yakapunguze changamoto mbalimbali ikiwemo ya usafiri wa kumpeleke wanafunzi pindi wanapougua wakiwa shuleni,” amesema Mwambe.
Amesema magari hayo yametolewa kwa shule tatu za shule za kutwa za Masasi, shule ya Wasichana ya bweni ya Masasi pamoja na shule ya Anna Abdalah.
Amezitaka shule hizo kutunza magari hayo ili yaweze kusaidia katika shule hizo.
“Kwa dhati kabisa ninapenda kutoa rai mukayatunze magari haya kwa kuwa wanufaika wa magari haya ni sisi wenyewe, tuuenzi ule msemo wa zamani wa kwamba chako kitunze ili kije kunufaisha na wengine hapo baadae,” amesema.
Aidha Mwambe ameainisha kuwa mbali ya magari hayo Serikali katika bajeti yake imetenga sh. Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari jimboni hapo.
“Wakati huu nakabidhi magari haya napenda niwaeleze kuwa tumetengewa pia fedha takribani sh. bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari hapa hivyo ili ni jambo la kujivunia na lenye kuleta sura mpya ya matarajio chanya kwa jimbo letu”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Claudia Kitta amempongeza mbunge huyo kwa jitihada zake anazozifanya za kuleta maendeleo katika jimbo hilo na kuwaomba wakazi hao kumpa ushirikiano mbunge huyo ili kufanikisha azma ya Serikali kuleta maendeleo katika mji huo.
“Mimi kipekee kabisa ni chukue fursa hii kukupongeza mbunge wetu kwa jitihada zako na kwa kweli matunda yake tunayaona na niwaombe ndugu zangu tumpe ushirikiano wa kutoka mbunge wetu kwa kuwa ameonesha nia ya kutuletea maendeleo ya kweli,”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari ya kutwa ya Masasi, Emmanuel Kumira, akizungumza kwa niaba ya wakuu wengine wa shule hizo zilizokabidhiwa magari hayo, amemshukuru mbunge huyo kwa kuwakabidhi magari hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yatakwenda kusaidia kutatua changamoto za usafiri pindi wanafunzi wanapohitaji kukimbizwa hospitalini.
“Kwa niaba ya walimu wenzangu, ninapenda nitangulize shukrani zangu moja kwa moja kwako mbunge wetu kwa kutupatia magari haya ambayo yatakuwa chachu na sehemu ya maboresho ya elimu katika shule zetu,” amesema.
Magari hayo ni miongoni mwa ahadi za mbunge huyo kwenye kuboresha sekta ya elimu katika jimbo hilo huku pia akianisha mipango mbalimbali kwenye kuboresha sekta ya afya, maji, miundombinu na nishati katika jimbo hilo.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi