January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani, Jumaa Aweso akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru baada ya kuwasili wilayani Pangani. (Picha na Hadija Bagasha).

Waziri Aweso atoa ombi kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2021

Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online Tanga

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani amemuomba kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Josephine Mwambashi asisite kukagua miradi ya maji nchi nzima kwa kuwa ripoti yake itasaidia kuchukua hatua mbalimbali ili kuweza kukamilisha miradi ya maji nchi kama ilivyo azima ya Rais ya kumtua mama ndoo kichwani iweze kutimia.

Waziri Aweso ameyasema hayo wakati kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru alipokuwa wilayani Pangani mkoani Tanga ambapo alisema kitendo cha kukagua miradi ya maji itasaidia kuchukua hatua za kukamilisha miradi mvalimbali nchini.

Waziri Aweso amesema, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania amempa dhamana ya kuhakikisha watanzania wanaondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama nchini,hivyo atahakikisha anawatua kina mama ndoo kichwani.

“Ndugu zangu watanzania nimepewa dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama hii dhamana ni kubwa sana hivyo nikuombe kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa usisite katika kila wilaya na mikoa kukagua miradi ya maji inayotekelezwa nchini, “alisisitiza Waziri Aweso.

Ukiwa wilayani Pangani Mwenge wa Uhuru ulikagua miradi 7 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 ikiwemo wa maji Kijiji cha Mikocheni Kata ya Mkwaja.

Akizungumza baada ya mwenge kuweka jiwe la msingi, kukagua na kupitia miradi hiyo 7 kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Josephine aliridhishwa na miradi ya Pangani na kuwataka viongozi pamoja na wananchi wa wilaya hiyo kufanyia kazi ujumbe wa Mwenge unaoelezea matumizi sahihi ya TEHAMA, chini ya kauli mbiu isemayo “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu .Itumie kwa usahihi na Uwajibikaji”.

Alisema, miradi waliyoipitia iwe endelevu sababu inaleta maendeleo ya Taifa na kusaidia kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.