May 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Aweso atoa maelekezo kwa Wakurugenzi huduma za maji nchini

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ameagiza  vitengo vya huduma kwa wateja vya Mamlaka za Maji nchini kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda na maeneo ya hifadhi  ili ikitokea changamoto wawe na uhakika wa kupata rasirimali hiyo.

Aweso ametoa maelekezo hayo leo  Mei,28,2025 wakati akizungumza na wakurugenzi na mameneja wa huduma kwa wateja  katika kikao  kazi cha  siku tatu kinachofanyika ukumbi wa Tughimbe Jijini Mbeya.

“Tuwape mbinu sahihi wananchi namna ya matumizi yasahihi ya maji na kuyahifadhi rasirimali hiyo ili kusaidia wananchi kuondokana na hadha ya huduma hiyo inapo jitikeza hitilafu,”amesema.

Ameongeza”Mamlaka inapata hitilafu ndogo tu wananchi wanahaha,lazima mtengeneze uhamasishaji na uhifadhi wa vyanzo na elimu itolewe kwa jamii,”amesema.

Aweso amewasisitiza kuwa wakurugenzi wa huduma kwa wateja kujenga uaminifu na kwa wateja kwa kutenda kazi kwa wito.

“Mimi nimewahi kuulizwa kuwa mbona wewe ni Waziri tunakuona unabeba ndoo za maji kichwani.Hivi jamani hutakuwa mkulima bila kubeba jembe kwenda shambani,lazima uipende kazi hamna kazi nyingine,kama huduma siyo nzuri hapo hakuna ukurugenzi niwaombe wakurugenzi moja ya jambo  msingi ni kuipenda kazi na ukishaipenda  kila kitu kitaenda vizuri”amesema Waziri Aweso.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Mhandisi Mwajuma Waziri amesema  matarajio ya wateja ni kupata huduma bora na kuwapongeza Wakurugenzi wa huduma za maji nchini kwa  jitihada wanazofanya katika kutoa huduma wananchi.

“Lakini bado hamjafika kwenye huduma bora bado mpo kwenye matarajio ya wateja,niwapongeze kwa “kauli mbinu hii lakini bado kuna changamoto nyingi ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi”amesema Mhandisi Waziri.

Mhandisi Waziri amesema kuna tatizo la kuna upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambayo yanasababishwa na wakurugenzi wenyewe na watu waliopo chini yao kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Mkurugenzi Msaidizi wa Usambazaji wa Huduma za  Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya Maji,Nasra Mduma , amesema katika kikao kazi hicho wameweza kushiriki mijadala yenye tija wakiangazia mada muhimu kama mbinu za kuthibiti  madeni uboreshaji wa huduma kwa wateja kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), na  mikakati ya kukabiliana na tatizo la  kupunguza upotevu wa maji.

Amesema kuwa kitu kingine walichojifunza ni tatizo la  afya ya akili kwa watendaji na utafutaji wa vyanzo mbadala vya fedha kwa uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za mamlaka hapa nchini.