Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega, amewasilisha bungeni bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026 akiomba Bunge limuidhinishie jumla ya Shilingi Trilioni 2.28 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, usalama barabarani, mazingira na udhibiti wa uzito wa magari.
Katika hotuba yake Leo Mei 5,2025 Bungeni jijini Dodoma,Ulega aliweka msisitizo mkubwa kwenye usalama barabarani, akieleza hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali kupitia TANROADS.
Alieleza kuwa ukaguzi wa usalama wa barabara umefanyika nchi nzima na maeneo hatarishi kubainishwa kwa ajili ya maboresho. Aidha, taa za barabarani na alama muhimu zimewekwa katika maeneo mbalimbali ya mijini ili kupunguza ajali.
Katika kukabiliana na ajali zinazotokana na uchovu wa madereva, Waziri Ulega alieleza kuwa Serikali inajenga maeneo maalum ya kupumzika kwenye kanda kuu za usafirishaji nchini. Vituo vya mapumziko vinajengwa katika mikoa ya Singida, Morogoro, Songwe, Kagera, Kilimanjaro na Pwani.
Waziri Ulega pia alieleza kuwa elimu ya usalama barabarani imetolewa kwa wananchi zaidi ya 18,000, huku TANROADS ikishinda tuzo ya kimataifa ya ‘iRAP Gary Liddle Memorial Trophy’ kutokana na juhudi zake za kuboresha usalama wa barabara.
Katika kudhibiti uzito wa magari,amesema Serikali inaendelea kujenga mizani za kisasa 32 katika mikoa mbalimbali pamoja na kufunga mfumo wa kupima magari yakiwa katika mwendo (WIMS).
Kwa mujibu wa Waziri huyo,Ujenzi wa mizani ya kisasa umefikia hatua mbalimbali huku usanifu wa kufunga kamera za CCTV katika mizani 58 ukiendelea.
Pia, hotuba hiyo iligusia ushirikiano mpya wa kiufundi kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la JICA la Japan katika kuboresha mfumo wa usimamizi wa usalama barabarani kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Aprili 2025.
Kwa upande wa mazingira, Waziri Ulega alieleza kuwa Wizara imepanda miti 166,635 katika hifadhi za barabara nchini kote, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupendezesha mazingira.
Katika sekta ya anga, Ulega alieleza maendeleo ya miradi ya viwanja vya ndege kumi, ikiwemo ujenzi unaoendelea wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato, ambapo sehemu ya kwanza ya ujenzi imefikia asilimia 87.
Aidha alisema,viwanja vingine vinavyoendelea na ukarabati au uboreshaji ni pamoja na Kigoma, Tabora, Sumbawanga, Shinyanga, Musoma, Iringa, Geita, Tanga na Lake Manyara.
More Stories
CCM kusimamia kitabu cha Hayati Songambele kiingie mtaani
Mwendokasi kuendeshwa na ENG kwa miaka 12
Vitongoji 284 Arumeru Mashariki vyafikiwa na umeme