January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee watakiwa usimamia maadili ya watoto


Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rungwe


Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee Taifa Anyimike Mwasakilali amewataka wazee kupitia umoja wao kulisimamia suala la maadili kwa watoto wao ili kuwa na taifa linalo. heshimika duniani kwa kuwa na watu waliostaarabika.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema kuwa jamii sasa imepoteza mwelekeo ambapo kumekuwa na mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana huku wenye uwezo wa kuirudisha jamii katika misingi yake ni wazee.


Amesema umoja wa Wazee kitaifa umesajiliwa kama taasisi ya kushughulikia masuala yanayowagusa wazee nchini lakini pia wanalo jukumu la kuhakikisha mambo katika taifa yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kukemea pale inapoonekana kuna jambo linakwenda kinyume na ustawi wa taifa.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa wazee nchini wanakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na hilo wameamua kuanzisha taasisi hiyo ya Wazee itakayowaunganisha na kuwa na nguvu ya pamoja kupigania haki zao ikiwa ni pamoja na masuala ya kijamii.


Hata hivyo ameeleza kuwa tangu taasisi hiyo isajiliwe na kuanza kufanya kazi nchini Oktoba 23,2023 na makao makuu yake yakiwa wilayani Rungwe wamefanikiwa kuwaunganisha wazee nchi nzima pia wameweza kuyashughulikia baadhi ya mambo kama vile soko la parachichi Rungwe ikiwa ni pamoja na kushirikiana na viongozi wa serikali katika kusukuma ajenda mbalimbali zenye maslahi kwa taifa.


Julius Kitao mkazi wa kijiji cha Muze mkoani Rukwa amedai kuwa kuna mambo mengi walikua wakishindwa kuyakabili kama wazee lakini umoja huo umewapa nguvu.


Anganile Sanga mmoja wa wazee kutoka wilayani Makete mkoani NJombe amedai kuwa umoja huo umefanikiwa kuwakutanisha wataalamu wa kada mbalimbali ambao ni wastaafu na kuwa imewasaidia sana kushughulika na changamoto wanazozipitia na kupata suluhisho.