December 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee waliopigania Uhuru kufanyiwa dua siku ya Maulid

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA),Mkoa wa Mwanza,katika kuadhimisha siku ya Maulid itakayofanyika kimkoa katika Msikiti Mkuu wa Wilaya ya Magu,imeiagiza misikiti yote mkoani humu,kufanya dua maalum kwa ajili ya wazee,waliojitoa kupigania Uhuru wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Desemba 3,2024, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke, amesema a Sherehe za Maulidi zitakazofanyika Desemba 8, mwaka huu Msikiti Mkuu wilayani Magu.

Ambapo amesema adhuhuri ya siku hiyo misikiti yote mkoani Mwanza,ifanye dua maalumu ya kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,wazee waliojitoa kupigania Uhuru pamoja na kuiombea nchi amani.

Pia amesema,taasisi hiyo itatumia sherehe za Maulidi kupanda miti ili kutunza na kulinda mazingira,kuchangia damu kwa ajili ya kusaidia hospitali na vituo vya afya,akiba ya damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji ikizingatia damu haina kiwanda.

Katika hatua nyingine BAKWATA imelaani matukio ya ukatili yakiwemo ya ulawiti,ubakaji,mauaji na unyanyasaji wa kijinsia,hivyo imewataka viongozi na wamiliki wa madrasa na markazi kuzisimamia kwa weledi zisiwe chanzo cha matukio hayo mabaya katika jamii.

Sanjari na hayo,Sheikh Kabeke amevishukuru vyama vya siasa kwa kuonesha utulivu,kwani watu walidhani kungetokea viashiria vya uvunjifu wa amani wakati wa kutangaza matokeo katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27,2024.