December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee waiomba serikali kusamehe kodi za majengo

Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya

WAZEE Jijini Mbeya wameiomba serikali kusamehe kodi za majengo ambayo sio za biashara kutokana na baadhi yao kuwa na hali duni za maisha ambazo zinasababisha kushindwa kumudu kulipa na kupelekea kuwa na malimbikizo ya madeni.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 3,2024 na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Mbeya,Hezron Kapwela wakati akizungumza na mwandishi wa habari kuelekea siku ya wazee Duniani ambayo ufanyika kila Oktoba Mosi kila mwaka.

Amesema malipo ya kodi za majengo imekuwa kero kwa wazee wasiojiweza na kuomba serikali kuliangalia upya ili kuweza kuwasaidia kwani idadi kubwa wanaoishi mazingira magumu .

“Kuelekea maadhimisho ya siku ya wazee duniani tunaomba serikali na wawakilishi wetu bungeni kusamehe kodi za majengo ambazo si za biashara unakuta mzee amejenga nyumba yake anaishi lakini anakwata kodi anaponunua nishati ya za umeme suala hili limekuwa ni kero “amesema.

Ameongeza kuwa“Kila wanapofanya mikutano wazee wanalalamika na hatua inayotumika kuandika barua Mamlaka ya mapato ni ndefu na ni gharama kwa mzee anayeishi kijijini kutokana wengi wao umri kuwa mkubwa kupata fedha ni tatizo hivyo tunaomba serikali izingatie”amesema mzee Kapwela.

Kuhusu vijana wanaotelekeza wazazi wao na kuwaachia mzigo wa kulea wajukuu wameombwa itungwe sheria ya kuwabana ili kuwatunza huku asilimia kubwa ya wanaoishi vijijini wanakaa na wajukuu hivyo ni serikali iangalia suala hili na kupitisha sheria bungeni ili iendelee kupunguza matatizo kwa Tanzania kuelekea 2030.

Wakati huo huo ameomba kuingizwa kwenye vyombo vya uwakilishi na kuwa wajumbe halali ili kujadili ukatili wanaofanyiwa dhidi yao wa kuporwa mashamba , mifugo, mazao yaliyolimwa ambayo uporwa na vijana bila kuwashirikisha wazazi ,pamoja na kuomba kuwa na mwakilishi wa wazee bungeni ambaye atazungumza mambo ya wazee.

Kwa upande wake Katibu Baraza la ushauri la wazee Mkoa wa Mbeya,Said Mwapongo amesema serikali ikatunga sheria sera iliyopo imetungwa 2003 na kwamba sera hiyo ipo zaidi ya miaka 20,bado sheria haitungwi na ni muda mrefu ambayo haitoi matumaini kwa wazee.

Amesema sheria waliotunga sera hiyo hawapo kwenye uhai na waliopo kwenye uhai wakaona sheria ya wazee,lakini wapo wazee waliotumikia Taifa kwa muda mrefu kwa shughuli zao mbali mbali huku wengi hawana uwezo wanaishi maisha ya chini ni vema serikali ikaanzisha pensheni kwa wazee kwa ajili ya kuendesha kwa ajili ya kujikimu kama ilivyo Zanzibar .

Aidha Mwapongo amesema kanuni mpya za bima ya afya zikumbuke kundi la wazee ambao wanapatiwa matibabu bila malipo kwenye vituo vya afya na Zahanati na kwamba bahati mbaya magonjwa yaliyo mengi hayatibiwi kwenye hospitali za wilaya, mkoa pamoja na Rufaa ambapo bima walizonazo haziwezi kufanya kazi ni vema Taifa ikaendelea kuimarisha na kuzitungia kanuni mpya kwa bima walinazo ili ziweze kutumika kwenye hospitali za wilaya ,mkoa na kanda.

Akielezea zaidi Mwapongo wamesema idara ya ustawi wa jamii izidi kujipambanusa ili wazee waweze kunufaika kupitia idara hiyo kwa kuwa idara inayojitegemea na kuwa na bajeti zake ili wazee wanufaike,pamoja na sera ya Taifa ya wazee 2003/2019 itungiwe sheria kutokana na sheria iliyopo kuwa ya muda mrefu.

Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji wa shirika la( RADO )ambalo linajishughulisha na masuala ya wazee,Musa Mcharo amesema kuelekea siku ya wazee ameikumbusha Serikali kuendelea kulikumbuka kundi la Wazee hasa wale waishiyo pembezoni Vijijini kwa kuwaboreshea huduma za msingi.

Hata hivyo Mcharo amesema kuwa kupitia bunge ikumbuke kutunga Sheria ya Wazee ambayo itaboresha mustakabali na maisha ya Wazee na kuangalia wa kutoa pensheni hasa wazee waliokuwa hawajaajiriwa kwenye sekta rasmi hata kwa wenye umri wa miaka 70, kwa kuweza kuchagua pia hata eneo dogo la kuanzia.

Akielezea kuhusu kodi za majengo,serikali iangalie mchakato rafiki wa kuwawezesha wazee wenye majengo wanayoishi yatolewe kwenye mfumo wa kulipa kodi za majengo ile inayolipwa sasa kupitia ununuzi wa umeme maarufu kama Luku. Wazee wengi wamechoka na pia nguvu za kuingiza kipato zimepungua sana.