January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee Shinyanga waomba sheria kali kudhibiti mmomonyoko wa maadili

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga

BARAZA la Wazee Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini,imemuomba Rais Samia kuweka sheria kali kudhibiti mmomonyoko wa maadili ambao unaendelea nchini.

Ombi la wazee hao limetolewa mbele ya waandishi wa habari na Makamu Mwenyekiti wake, Zengo Mikomangwa,ambapo ameeleza kuwa kuhusu suala la mmomonyoko wa maadili (ushoga) wazee hao wamelaani vikali vitendo hivyo.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Zengo Mikomangwa.

Ambapo wamewaomba watanzania wote nchini kuunganisha nguvu zao kupinga vikali vitendo hivyo visipate nafasi ya kuota mizizi na kuleta athari nyingi hasa kwa vijana wanaochipukia hivi sasa.

“Tuna mashirika mengi sana (NGO’s) yanayosajiliwa na kudhibitiwa na Serikali lakini tunasikitika yanafanya vitendo hivi na Serikali ikiangalia aidha kwa makusudi au kwa kutokujua hatuwezi kumuhukumu mtu au kwa kupewa chochote kile ili wazibe masikio pamoja na macho yao, lakini wananchi wanaona,”.

Hivyo wamemuomba Rais kusikia kilio hicho na achukulie kwa umuhimu wa pekee kwa kuangalia sheria za nchi, na kama zina ulegevu aliagize Bunge litafute sheria ambazo zitawabana wahusika na hazitaruhusu kabisa suala la ushoga ili wasije kupoteza kizazi chao.

Wajumbe wa Baraza la wazee wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Sanjari na hayo wametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa ambazo amezifanya ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.

Ambapo wamesema ndani ya kipindi hicho cha miaka miwili, Rais Samia ameweza kuendeleza miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake Hayati John Magufuli na kuanzisha miradi mingine mipya.

Amesema miradi yote inayoendelezwa na mipya iliyoanzishwa yote inakwenda kwa kasi ya ajabu na kila mmoja anaona hasa kwenye maeneo ya usafirishaji, afya,shule pamoja na demokrasia ambapo ametoa uhuru kwa vyama vyote vya siasa kwa ajili ya kujenga nchi yenye uimara, umoja na ushirikiano ili nchi iwe na amani wakati wote.

Pia amesema pongezi hizo zinakwenda pamoja na kumuomba Rais Samia ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa, aendelee kufanya usamimizi imara wa raslimali zote za nchi, hii ni pamoja na raslimali watu na raslimali fedha.

Ameeleza kuwa kuna baadhi ya wasaidizi wake wamekuwa hawawajibiki katika kutunza raslimali za nchi utendaji wao wa kazi umekuwa wa kusuasua, na isitoshe na la kusikitisha kabisa ni ufujaji wa fedha ama kutumia vibaya fedha bila kuzingitia misingi ya sheria ya matumizi ya fedha.

“Hili limekuwa likiwasikitisha sana wazee na wananchi wote wapenzi wa CCM na wasiokuwa wanachama kwamba fedha nyingi imefujwa ama kutumika nje ya utaratibu, hasa baada ya kutolewa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG),” ameeleza.

Wazee hao wamemuomba Rais Samia atumie taratibu zote za kiutawala na kisheria za kuwadhibiti wale wote wanaofuja kabla hawajafuja na watakaothibitika kwamba wamefuja bila kujua au kwa kujua kwa vile kuna sheria ya usimamizi wa fedha basi wachukuliwe hatua za kisheria ama adhabu zinazostahili kwa mujibu wa sheria.

Wamesema taratibu zote za kisheria zifuatwe bila kumuonea wala kumpendelea au kumdhulumu mtu lakini haki ya watanzania wanaitaka kabla hawajaidai kwa njia yoyote ile huku wakimuomba Rais alichukulie suala hilo kwa uzito unaostahili bila ya mhemko wala jazba na atulie aiache sheria ifuate mkondo wake.