March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee Buyuni kunufaika na bima za afya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

Imeelezwa kuwa  Kata ya Buyuni, imefanikiwa kutekeleza hatua mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo kuazisha zoezi la kuwapatia wazee bima za afya ili waweze kupata huduma salama katika vituo vya  afya.

Hatua hiyo ni ndani ya siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuapishwa baada ya kumaliza kwa uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025.

Diwani wa Kata ya Buyuni,Jesca Msolla ameyabainisha hayo Jijini Dar-es-Salaam Januari 15,2026 wakati akizugumza na waandishi wa habari ambapo amesema Kata hiyo ina jumla ya mitaa nane,

 “Wenyeviti wa mitaa hii nane tayari wameanza kuratibu zoezi la kuwabaini wazee wote wanaohitaji bima za afya, hatua inayolenga kuhakikisha wanapata huduma za matibabu bila vikwazo,”amesema Msolla.

Akizungumzia fursa za kiuchumi, amesema Rais Samia  kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar -es-Salaam ametoa maelekezo kwa Watendaji wa Kata na Wenyeviti wa Serikali za mitaa kuhusu utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10, ambayo tayari imetolewa ikiwemo kwa Kata ya Buyuni.

Amesema, kata hiyo imeanza kuvitambua na kuvisajili vikundi vyenye sifa ya kunufaika na mikopo hiyo, inayolenga makundi ya wanawake, vijana na  watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuwawezesha wananchi hao kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Diwani huyo amesema mchakato wa ujenzi wa shule kwa ajili ya watoto wa makundi maalumu umeanza rasmi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya  kuhakikisha watoto wote wanapata haki ya elimu bila ubaguzi.

“Nashukuru uongozi wa Wilaya ya Ilala ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, kwa kuweka kipaumbele katika kusikiliza na kushughulikia mahitaji ya Kata ya Buyuni, hali inayochochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo hili,”amesema. 

Pia amesema,kata hiyo  imepewa kipaumbele cha kujenga shule kubwa ya ghorofa kwa ajili ya kuongeza idadi ya madarasa, mradi unaolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia, huku fedha za utekelezaji zikiwa tayari zimetengwa.

Kwa upande wa sekta ya afya, amesema zahanati ya Buyuni imeboreshwa na kupandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya Buyuni, ambacho kipo katika hatua za mwisho za kukamilika na kinatarajiwa kutoa huduma za mama na mtoto pamoja na huduma za upasuaji kwa wajawazito wanaopata changamoto wakati wa kujifungua.

Amesema uboreshaji huo utasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi, huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kuzingatia afya ya mama mjamzito na mtoto chini ya miaka mitano.

Akizungumzia suala la ulinzi na usalama, amesema kata hiyo imeimarisha ulinzi shirikishi kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Mitaa, Jeshi la Polisi na wananchi.