November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi,walezi watakiwa kuwalinda watoto

Na Mwandishi wetu, timesmajira

WAZAZI na Walezi nchini wameaswa kuwalinda watoto wao katika maadili na kusimamia malezi yao katika maisha ya uhalisia na kuacha kuiga tamaduni,mila na desturi za watu wengine.

Rai hiyo imetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Muasisi Shule Huria ya Ukonga Skillfull, Diodorus Tabaro wakati wa mahafali ya 15 ya shule hiyo,alisema miaka ya sasa wazazi na walezi wengi wamekuwa wakiwadekeza watoto wao maisha hali inayowafanya watoto kutokuwa wakakamavu kama miaka ya nyuma.

Amesema suala la maadili sasa hivi limekuwa janga kubwa kimataifa hivyo ni lazima wapigane nayo kuhakikisha wanawalinda watoto wao katika maadili yaliyomema na mazuri ambayo yatakuja kuwaletea tija miaka ya baadae wanapokuwa wakubwa.

”Wazazi muache kuwadekeza vijana wenu,mkae nao na kuhakikisha mnawalea katika maadili yaliyomema muache kuwadekeza kwani vijana wa sasa wanaishi maisha feki ,mzazi au mlezi usimshindwe mtoto wako unapaswa kumwambia ukweli,”amesema na kuongeza

”Tujitahidi kuwalea watoto wetu katika misingi mizuri,kwani hata hizi tabia zinazotoka huko nchi nyingine na kuingia nchini ndo hizi zinazowaharibu watoto wetu,”amesisitiza.

Amesema wazazi wengi wameshindwa kufanya jukumu la malezi kwa kutokuwa karibu na watoto wao, wengi wakikimbizana na jukumu la kutafuta fedha jambo ambalo wakati fulani linawapa wakati mgumu walimu kuwa karibu na watoto kama walivyo wazazi.

“Ni muhimu wazazi kutumia muda mwingi kuwa karibu na watoto wao, mnapowapeleka shuleni zingatie kuwafatilia kila hatua yanayopitia hiyo itasaidia hata katika ufahulu wao, tumieni muda huo kuwaonyedha pia uhalisia wa maisha jinsi ulivyo, wasijaribu kuishi maisha ya mitandaoni yaani fake life ambayo kwa sasa ndiyo yanawatesa vijana wengi nchini,” alisema

Aidha Tabaro amewataka wazazi na walezi kutowakatia tamaa vijana wao walioshindwa kupata alama nzuri za ufaulu katika mitihani ya kitaifa badala yake watafute njia za kuwasaidia ili waweze kutimiza ndoto zao.

Amesema katika shule hiyo ambayo inadahili wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na wale walioshindwa kuendelea na masomo na kushindwa kufanya mitihani ya taifa wamekuwa wakikutana na changamoto za wanafunzi waliokata tamaa ya kuendelea na masomo lakini walimu wa shule hiyo wamekuwa wakiwatia moyo ili waweze kufikia ndoto zao.

”Hatuna budi kuwatia moyo watoto hawa kwani safari yao ndo imeanza rasmi,tumeishi na wanafunzi hawa kwa kipindi cha mwaka mmoja na tumewapika kimaadili,Kimalezi na Kimasomo tunaamini wanapoenda kuanza mitihani yao watafanya vizuri kwa kupata alama A na B,”amesema.

Awali akiongea na Wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita katika shule hiyo,Wakili na Mkufunzi Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam Eva Mosh, amesema wazazi waache tabia ya kuwachagulia watoto wao nini waende kusoma badala yake wakae chini na watoto na kuwasilikiliza fani gani mtoto anapenda kwenda kuisomea akiwa elimu ya vyuo vikuu.

Amesema Wazazi tumekuwa tunawaangusha watoto wetu kimasomo kwa sababu tunawachagulia vitu vya kwenda kusoma wanapokuwa vyuo vikuu ambavyo wao hawataki kuvisoma,hali inayofanya kutofikia ndoto zao na kusababisha wao kufeli masomo,”amesema na kuongeza

”Hizi taaluma za zamani tusizing’ang’anie kwani sasa hivi kuna fani nyingi tu,mtoto anaweza akachagua mwenyewe kitu ambacho anakipenda kukifanya,unapomchagulia mtoto fani na kuvamia fani hiyo unasababisha kutengeneza tatizo kubwa la watoto kufeli masomo na kutofikia malengo yao,”amesema.

Naye Mwanafunzi anayemaliza kidato cha sita katika shule hiyo,Ritha Mahunda amesema vijana walioshindwa mitihani yao ya taifa wasikate tamaa kwani Ukonga Skillfull ipo kwa ajili ya kuweza kutumiza ndoto zao walizojiwekea.

Alphani Hamissi ambaye ni miongoni mwa wazazi wa watoto wanaosoma shule hiyo amesifu jitihada za walimu katika kuwafundisha wanafunzi waliopo kwenye shule hiyo kwani wanajitahidi kuhakikisha wanawafundisha vema na kuwa maendeleo mazuri yakielimu.