Na Mwandishi wetu,Timesmajira
MWENYEKITI wa Umoja wa Wakuu wa Shule Nzega Vijijini,Jumanne Shaban amesema wazazi wilaya hiyo wameanza kutumia mfumo mpya wa kuwaozesha watoto wao wa kike katika umri mdogo kwa kuwalazimisha kufanya vibaya katika mitihani yao ya taifa kwa kisingizio cha kuwatafutia kazi mjini.
Amesema wamebaini hayo kutokana na kupokea kero nyingi kutoka kwa wazazi namna wanavyowarubuni wanafunzi wa kike kufanya vibaya katika mitihani hiyo kwa lengo la kuwa wametafutiwa kazi nzuri na ndugu ambao wanaishi nao mbali kumbe ni njia ya kumuozesha mtoto akiwa na umri mdogo.
Akizungumza jana Mkoani Tabora wilayani humo,wakati walipotembelewa na Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni(TECMN),katika Kijiji cha Isagenhe ambapo Taasisi ya Msichana Initiative imekuwa ikifanya nayo kazi tangu mwaka 2022 katika miradi mbalimbali ikiwemo Majukwaa ya kutoa elimu ya ndoa za utotoni (Msichana Cafe),Arudi Shule, Klabu ya Msichana Amani pamoja na Mradi wa Baiskeli moja,Msichana mmoja.
Amesema kwa sasa wazazi wamekuwa wanawaozesha watoto wao wa kike kwa usiri mkubwa na kutumia njia mbalimbali za kuwarubuniwa ili wazazi wao kwa manufaa yao ya kupata mali.
”Kuna wakati utaona maendeleo ya mtoto yanabadilika labda alikuwa anapata ufaulu mzuri katika mitihani yake lakini kadri muda unavyoelekea katika mtihani wa Taifa unashangaa kuona mtoto anashuka kitaaluma.
”Ukimuhoji mtoto kwanini anashuka kielimu unakuta anakuambia hakuna tatizo ambapo wanaweka usiri mkubwa na ukienda mbali zaidi kuwauliza watoto utasikia,hawatumii yale maneno ya mojamoja ya uelewa wanachokifanya wazazi au walezi wanawaelekeza watoto kwamba waache shule kunakazi nzuri za kufanya,”amesema na kuongeza
”Ukitoka hapa utaenda kwa mjomba ako ukafanye kazi nzuri, sasa ili uweze kwenda inabidi ujifelishe katika mitihani yako ya taifa hizo ndio njia wanayotumia na sio tena kumwambia utaenda kuolewa moja kwa moja,”amesema Mwalimu
Amesema kwa kiasi kikubwa wanakumbana na kesi hizo hivyo wao kama wataalamu wanachokifanya ni kuwashauri watoto kisaikolojia na kuwaita wazazi wao na kuzungumza nao ikishindikana kabisa tunawasilisha taarifa hizi katika mamlaka za kisheria.
Kwa Upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Isagnehe,Alex Madale amesema kuozesha mtoto wa kike kwa watu wa Tabora imekuwa kama ni desturi kwao,kuona mtoto wa kike kazi yake sio kusoma bali ni kuolewa.
”Mzazi anapokuwa amejipatia mtoto wa kike basi anajua anamali na tayari hapo anatoa umasikini kwa kusema amejipatia mkulima maana yake amejipatia mali,”amesema.
Alisema sasa ni wakati wa kuwatendea haki watoto wa kike kwa kuacha wapate elimu ili waweze kutimiza ndoto zao ambazo wao wenyewe wanaona wataziishi.
Naye Afisa Miradi wa Wilaya ya Nzega Taasisi ya Msichana Initiative,Rosemary Richard alisema kuna changamoto nyingi kwa wasichana wa wilaya hiyo wanazozipitia ikiwemo ya ndoa ya utotoni.
”Kutokana na changamoto hizi tumekuwa na miradi mbalimbali tunayoifanya kama shirika ikiwemo mradi wa Klabu za Msichana za Amani ambazo zinafanyika katika kata 10 katika shule za msingi lengo likiwa kuwajengea watoto kujitambua,kujisimamia wenyewe na kupinga vitendo vya ukatili,pia tunamradi wa Arudi Shule kupitia muongozo wa serikali uliotolewa wa kuwarudisha watoto walioacha shule kwa sababu mbalimbali ambapo tumefikia wasichana 200 na kutoa michango kama sale za shule pamoja na Mabegi,”amesema.
Richard amesema moja ya changamoto kubwa wanayokutana nayo watoto wa kike ni pamoja na wazazi wengi wamekuwa wakitumia kiburi cha kwamba asipokuwa anampatia mtoto mahitaji,mtoto ataacha mwenyewe kwenda shuleni kusoma na kufanya mzazi kutumia nafasi hiyo kumuozesha mtoto ili apate mali.
Ziara hiyo ikiwa ni muendelezo wa Mtandao wa TECMN chini ya mashirika 87 kati ya hayo mashirika sita yameweza kuwakilisha katika mikoa mbalimbali kukusanya maoni juu ya sheria ya mtoto ya mwaka 1971,Miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na Msichana Initiative,Binti Makini,Medea Plan Internationa,MyLegacy pamoja na Theatre Arts Femist Group.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo