Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar
WAZAZI na walezi wa watoto waliokuwa wakiishi na kufanyakazi mitaani wamepongeza kazi kubwa ambayo inafanywa na Railway Children Africa kwa kushirikiana na Taasisi ya Baba Watoto kwa kusaidia kuwaunganisha upya watoto hao na familia zao.
Taasisi hizo mbili zinatekelezam mradi wa USAID-Kizazi Kipya, ambao pamoja na mengine unaelimisha jamii iweze kutambua kuwa watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani wana mahitaji kama watoto kama wengine, hivyo wanahitaji kusaidiwa waweze kufikia ndoto zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni wazazi na walezi ambao watoto wamefanikiwa kurejeshwa kwenye familia zao, walisema kwa sasa ni mabalozi wazuri kwa jamii, kwani awali ilikuwa vigumu kutambua kama watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani wanaweza kubadilika na kurudi kwenye mfumo wa kawaida wa malezi ya watoto.
Akitoa ushuhuda wake mmoja wa wazazi mkazi wa Sinza D, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) amesema kabla mtoto wake kuondolewa kwenye mazingira ya kuishi na kufanyakazi mitaani taasisi hizo, tayari ndani ya familia walikuwa na ukakasi wa kuishi na mtoto huyo, ambaye kwa sasa amerudishwa nyumbani na anaendelea na masomo ya darasa la tatu.
“Huyu mtoto (jina linahifadhiwa) alikuwa na ukakasi wa kufanya tunachokitaka ilifikia hatua akawa ameoondoka nyumbani akaenda kuishi anakojua, lakini siku moja tulishangaa Railway Children Africa kwa kushirikiana na Taasisi ya Baba Watoto tuliona wanamleta hapa,” amesema baba wa mtoto huyo na kuongeza;
“Wametusaidia kutuelimisha namna ya kuishi naye ikiwa ni pamoja na kutusaidia kupata mahitaji muhimu ikiwemo ya shule na hata chakula…wameongeza uchangamfu kwenye familia yetu, kwani mtoto amebadikika.”
Amesema kupitia fundisho hilo,Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani hawapo huku kwa makusudi yao, bali kuna mambo yaliyowasukuma na yakipatiwa ufumbuzi wanarudi nyumbani na kutulia.
Ametoa mfano, akisema kama mtoto wake asingesaidiwa na taasisi hiyo anaamini mabadiliko ambayo wanayaishi sasa yasingekuwepo.
“Upendo ni kitu kikubwa kwa watoto, wanapokosa upendo wakati wowote watoto wanaondoka nyumbani kwenda kule ambako wanadhani upendo unapatikana na huo, unakuwa mwanzo wa kuishi na kufanyakazi mitaani,”alisema.
Amesema taasisi za aina hiyo zinastahili kuungwa mkono kwa nguvu zote kwa kutunga sera na sheria ambazo zinaweza kuwa rafiki katika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Kwa upande mama wa mtoto huyo (jina tunalo) alikiri kuwa watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani kuna sababu zinazowapeleka huko. Amesema kikubwa watoto wanahitaji upendo na hilo, ndilo jambo kubwa ambalo amejifunza kwa taasisi hiyo.
“Hata kama siku moja taasisi za aina kama hazitakuwepo, tutaendelea kuwa mabalozi wa watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani, tutakuwa jukwaa la kuwasaidia ili nao waondoke huko, kama alivyoondoka huyu wa kwangu,”amesema
More Stories
Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA
Mwanafunzi apoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba