Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
WAZAZI na walezi wametakiwa kuwa na utamaduni wa kuwapeleka watoto wao hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kama wana dalili yoyote ya saratani ya retina ili waweze kupata tiba mapema.
Huku wakihimizwa kuwapeleka kliniki watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ili wakapatiwe chanjo na kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba, Magonjwa yasiyoambukiza Wizara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu amesema hayo Mei 17,2024 kwenye maadhimisho ya wiki ya kuongeza uelewa kuhusu Saratani ya Macho kwa watoto “Retinoblastoma” yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.
Dkt.Ubuguyu amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchini zisizofanya vizuri kwenye saratani ya macho kwa watoto kutokana na uelewa mdogo unaosababisha wazazi kuchelewa kuchukua maamuzi ya kuwapeleka hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
Pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea na upanuzi pamoja na uboreshaji wa huduma za afya kwa kuongeza vifaa tiba, majengo na watumishi kwa lengo la kuzidi kuwasogezea huduma za hizo karibu zaidi na wananchi.
“Jitahidini kuwapeleka watoto kufanyiwa uchunguzi mapema ili waweze kupatiwa tiba mapema, kwani kupata tiba mapema kutaisaidia kujikinga na madhara makubwa ambayo wanaweza kupata,“amesema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt. Elizabeth Nyema aliyemwakilisha Waziri wa Afya Ummy p, kwenye maadhimisho hayo amesema Wizara ya Afya ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mradi utakaoenda kuboresha tiba kwa watoto hawa ili kuboresha uoni na kupunguza vifo vinavyotokana na saratani hiyo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia ngazi ya jamii hadi Hospitali za Kanda.
Ameongeza kuwa jumla ya wagonjwa wa saratani ya retina 227 walionwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa mwaka 2023 ukilinganisha na wagonjwa 214 walioonwa mwaka 2022 kwenye hospitali ya ngazi ya rufaa za Mkoa na Msingi.
Haya hivyo ametoa wito kwa wazazi kuwawahisha katika vituo vya kutolea huduma za afya watoto wao pindi waonapo dalili za ugonjwa huo.
“Idadi hii kubwa ya watoto wanafika kwenye hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa wakiwa kwenye hatua za mwisho za ugonjwa wa saratani ya Retina na kusababisha wengi wao kupoteza maisha, wazazi na walezi wawaisheni watoto hospitali mara baada ya kuona dalili za mwazo na kufuatilia tiba pindi tu wagundulikapo kuwa wana changamoto yoyote kwa maana uwezekano wa mtoto kupona na kuendelea kuishi baada ya kugundulika kuwa na saratani unategemea sana muda wa kufika hospitali,”amesema Dkt. Nyema.
Mkuu wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho Wizara ya Afya Dkt. Bernadetha Shilio amesema jumla ya watoto 120,000 walionwa mwaka 2023 kwenye kliniki za macho katika hospitali za Rufaa za Mikoa na ngazi ya Msingi kati yao asilimia 42 ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huku watoto takribani milioni 3.2 wenye umri wa chini ya miaka mitano walionwa katika kliniki za kawaida za ngazi za msingi.
“Magonjwa yaliyoongoza ni mzio kwenye macho, upeo mdogo wa macho unaorekebishika kwa miwani, maambukizi kwenye macho na asilimia 39 ni wenye matatizo ya macho yasiyoambukiza ikiwepo majeraha ya macho,”ameeleza Dkt. Shilio.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za afya nchini na ifikapo Oktoba mwaka huu huduma za matibabu ya saratani ya retina zitaanza kutolewa katika hospitali hiyo.
Ambapo tayari Serikali imewekeza kwenye vifaa tiba na jengo ambalo litasaidia kupunguza rufaa kwa watoto wenye saratani hiyo.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito