December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi watakiwa kutafuta taarifa sahihi za Malezi,makuzi ya mtoto mapema

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZAZI wameaswa kutafuta taarifa sahihi za malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto mara tu wanapofikiria kuanza kupata watoto ili kuwa na elimu ya kutosha itakayowawezesha kumlea mtoto katika maeneo muhimu na hivyo kumwezesha kukua na kufikia katika utimilifu wake bila vikwazo.

Hayo yamesema na Mratibu Kitengo cha Elimu ,ushauri na Msaada wa Kisaikolojia Taasisi ya Ustawi wa Jamii Rufina Khumbe katika maonyesho ya vyuo vya Ufundi Stadi na vyuo vya Kati yanayofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

“Malezi , makuzi na maendeleo ya awali ya awali ya mtoto  yanaanzia pale tu mama anapokuwa mjamzito,hivyo kwa wale wanaotaka kuanza kupata familia wanapaswa kutafuta taarifa hiz za malezi na makuzi ya mtoto mapema ili waweze kumlea mtoto atayaezaliwa katika maeneo yote muhimu ya ukuaji wake kwa lengo la kumwezesha kukua kwa utimilifu wake bila kuwa na vikwazo.”amesema,Khumbe na kuongeza kuwa

“Ni muhimu kuwe na mahudhirio ya kliniki kwa wazazi wote wawili kabla na baada ya mtoto kuzaliwa hadi anapofikisha umri wa miaka mitano  ,ili mtoto aweze chanjo zote zinazohitajika  na kuzingatia vyakula anavyotakiwa kula kulingana na umri wa mtoto.”

“Kliniki ndiko mtoto anafuatiliwa kwa karibu kwamba hatakiwi kula kitu chchote kwa kipindi cha miezi 6 zaidi ya kunyonya maziwa ya mama,na kama kuna shida yoyote basi matibabu ni bure kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano lengo ni kuhakikisha anapata huduma za afya bila kikwazo ili kuhakikisha malezi na makuzi yake katika umri huo hayakutani na kikwazo cha huduma za afya.”

Vile vile alisema,katika umri wa miaka 0-8 ndio eneo ambalo mtoto anachukua mafunzo kutoka kwa wazazi na jamii inayomzunguka kuanzia kwenye lugha inayotumika pamoja na mazingira yanayomzunguka.

Khumbe ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi Taasisi ya Ustawi wa Jamii amesema,jamii inapaswa kushirikiana kikamilifu katika malezi na makuzi ya mtoto pale anapoanza shule kwani ni eneo linalokuwa na changamoto kwa mtoto katika kujifunza mambo.

“Lakini mtoto huyo anapofika miaka minne anakuwa ameanza shule,sasa hapa shuleni mazingira yakoje na hapa kati kati anapotoka kwenda shule ,nyumbani na jamii,tunashirikianaje kumjenga huyu mtoto ili awe kijana mwenye kuleta tija kwa Taifa maana lishe ,matibabu,malezi afya na ulinzi  wa mtoto vinahusika .”amesema