December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi washirikishwe suala la upatikanaji madawati shule msingi

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga, ameeleza kuwa suala la madawati haliwezi kumalizwa na Serikali Kuu na halmashauri hiyo pekee.

Hivyo ametoa Rai kwa Kamati za Shule kuwashirikisha wazazi katika suala la upatikanaji wa madawati katika shule za msingi zilizopo ndani ya halmashauri hiyo,ili kutatua kero hiyo watoto wasome kwenye mazingira.

Mulunga ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela cha kujadili taarifa ya robo ya pili ya mwaka 2021/22,kilichofanyika katika halmashauri hiyo.

Pia amesema wenyeviti wa Serikali za mitaa waone umuhimu kuwashirikisha wananchi katika kutatua changamoto ya upungufu wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari wilayani Ilemela.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Marco Busungu,akisoma taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mhandisi Modest Apolinary,amesema Idara ya elimu msingi kwa mwaka 2022, ilijiwekea maoteo ya kuandikisha wanafunzi.

Ambapo kwa shule za awali wanafunzi 7,602 na wanafunzi 10,543 kwa darasa la kwanza.

Amesema hadi kufikia Februari wamefanikiwa kuvuka lengo la uandikishaji kwa darasa la kwanza kwa asilimia 110 na kwa darasa la awali wamefikia asilimia 79,ambapo uandikishaji unaendelea hadi Machi 31,2022.

Pia amesema,kwa upande wa elimu sekondari wanafunzi 10,640 walitarajiwa kudahiliwa, hadi kufikia Februari 17, wanafunzi 8,115 walidahiliwa ambapo kati yao wavulana 3,988 na wasichana 4,127 sawa na asilimia 76.3 wameripoti shuleni wanaendelea na masomo huku mapokezi ya wanafunzi yanaendelea hadi Machi 30,2022.

Sanjari na hayo alielezea suala la ujenzi wa shule mpya ya sekondari Buzuruga ambapo halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha milioni 470(470,000,000), Novemba 2021 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

“Hadi sasa miundombinu iliojengwa ni vyumba vya madarasa 8,maabara 3,maktaba 1,jengo la utawala,chumba cha komputa,matundu 20 ya vyoo na miundombinu ya maji,” amesema Busungu.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo cha kujadili taarifa ya robo ya pili ya mwaka 2021/22 kilichofanyika katika halmashauri hiyo. Picha na Judith Ferdinand
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Marco Busungu, akisoma taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela cha robo ya pili ya mwaka 2021/22 kilichofanyika halmashauri hapo. Picha na Judith Ferdinand
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela waliohudhuria kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo cha kujadili taarifa ya robo ya pili ya mwaka 2021/22 kilichofanyika katika halmashauri hiyo. Picha na Judith Ferdinand