January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi waonywa kuacha kupakia picha za watoto katika mitandao ya kijamii

Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Musoma

WAZAZI na walezi wametahadharishwa na kutakiwa kuacha kupakia mtandaoni maudhui za picha za watoto wao walio chini ya umri wa miaka 18 kwa kuwa jambo hilo linaweza kuhatarisha maisha yao baadae.

Ofisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Robin Ulikaye amesema hayo Aprili 13, 2024 Mjini Musoma mkoani Mara alipokuwa akiwasilisha mada katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na mamlaka hiyo kwa waandishi wa habari wa Mkoa huo.

Ulikaye amesema kuwa kumeibuka tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kupakia picha za watoto wao katika mtandao wa kijamii kwa dhamira njema lakini baadae inaweza kugeuka kuwa kaa la moto kwa watoto hao.

“Unaweza kupakia katika mtandao wa kijamii picha ya mwanao wa kike au wa kiume ukiwa na nia njema kabisa lakini kumbuka katika mtandao huo wapo wanaofanya biashara chafu kupitia picha au sauti wanaweza kugeuza picha hizo zikatumika vibaya au kuidukua na ‘ku-edit’ hiyo picha ya mwanao akaihusisha na udhalilishwaji wa kingono au uhalifu wa aina yoyote jambo litakaloweza kumchafua mwanao ndani ya jamii pindi anapokuwa mtu mzima,”ameeleza na kuongeza kuwa

“Mambo haya yanaweza yakafanyika kipindi ukiwa hai au baadae utakapokuwa umetoka duniani lakini kosa ulilofanya litabaki likimtesa mwanao kipindi chote cha maisha yake,”.

Amesema ni jukumu la TCRA kusimamia maudhui yanayorushwa mitandaoni kupitia vyombo vya kielektroniki hivyo ni vyema wakatoa tahadhari na angalizo kwa watanzania kuhusu mambo yanayoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa mitandao ya kijamii na mitandao mingineyo.

Amewataka waandishi wa habari kutumia taaluma zao katika kuelimisha jamii kuachana na tabia ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wao katika ulimwengu wa kidigitali.