Na Joyce Kasiki , Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imetoa onyo kali kwa watu binafsi na makampuni yanayojihusisha na uzalishaji haramu wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku pamoja na wanaoingiza bidhaa hizo kwa njia zisizo halali, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha ulinzi wa mazingira kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, alitoa kauli hiyo Leo Mei 27 jijini Dodoma wakati akitoa tamko rasmi la Serikali kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu yamebeba kaulimbiu: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo: Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki.”
“Serikali itaendelea kufanya doria za kushtukiza katika viwanda vilivyosajiliwa, viwanda bubu na maeneo ya masoko ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka sheria kwa kuzalisha au kusambaza mifuko ya plastiki,” alisisitiza Mhandisi Masauni.
Amezielekeza taasisi za usimamizi wa mazingira ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi nyingine za umma kuhakikisha zinaimarisha ufuatiliaji na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo vinavyohatarisha mazingira.
Aidha, Waziri Masauni amewakumbusha wananchi kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki na badala yake kutumia mifuko mbadala ambayo inapatikana kwa bei nafuu nchini kote, akisisitiza kuwa kulinda mazingira ni jukumu la kila Mtanzania.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2025 yatafanyika kitaifa jijini Dodoma kuanzia Juni 1 hadi 5 mwaka huu yakihusisha shughuli mbalimbali za kitaifa, ikiwemo mkutano wa vijana (Youth Summit) utakaowakutanisha vijana kutoka vyuo vikuu, wajasiriamali na mabalozi wa mazingira.
Katika kilele cha maadhimisho hayo Juni 5, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Kati ya shughuli kuu zitakazofanyika siku hiyo ni uzinduzi wa Taarifa ya Nne ya Hali ya Mazingira Duniani,uwasilishaji wa Mfumo wa Kidigitali wa Kupokea Taarifa za Mazingira kutoka kwa Wadau,utoaji wa Tuzo ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku na Tuzo za Utunzaji Bora wa Bustani za Kijani katika miji na majiji.
Alisema,Kimataifa, Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka huu itaadhimishwa katika Visiwa vya Jeju, Korea Kusini, chini ya kaulimbiu ya “End Plastic Pollution Globally” (Komesha Uchafuzi wa Mazingira unaochangiwa na Taka za Plastiki).
“Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha hatua za pamoja kukomesha uchafuzi wa plastiki duniani, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkataba wa kimataifa wa kudhibiti taka hizo.”alisema Mhandisi MasauniMaadhimisho haya yalianzishwa mwaka 1972 kupitia Mkutano wa Kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira uliofanyika Stockholm, Sweden, yakiwa na lengo la kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali asilia.
More Stories
Utabiri wa hali ya hewa saa 24 zijazo
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ashiriki ziara ya tume ya utumishi wa mahakama
Coca-Cola ‘chupa la machupa’ yapeleka ladha mpya Forodhani, Zanzibar