Na Mwandishi wetu .
WAZALISHAJI wa dawa wa viwanda vya ndani wamelalamikia namna ya utitiri wa kodi kutoka kwa mamlaka za Serikali huku pia wakieleza namna ya uhaba wa fedha za Kigeni hususani dola inavyowakwamisha katika ununuzi wa malighafi nje ya nchi
Hayo wamebainisha mapema Februari 19, 2024 wakati wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi, iliyoratibiwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini [TMDA] katika viwanda vya utengenezaji wa dawa vya wazawa ikiwemo kiwanda cha Kairuki na kiwanda cha Katwaza vyote vya Kibaha, Mkoani Pwani.
Awali Kamati hiyo, ilipokea taarifa ya utendaji kiwanda cha Kairuki na kutembelea kujionea uzalishaji wa kiwanda hicho.
Ellen Magita ni Meneja wa Kiwanda cha kuzalisha dawa cha Kairuki ambapo ameeleza kuwa, miongoni mwa changamoto yao kubwa ni ucheleweshwaji wa malipo kutoka Bohari ya Dawa nchini (MSD) hali inayowapa ugumu wa kununua malighafi kwa ajili ya uzalishaji zaidi.
Amebainisha kuwa, Mwaka 2018 wametumia Sh 60 bilioni katika kuanzisha kiwanda hicho, fedha ambazo ni mikopo ya benki za ndani na nje kama mdhamini huku wakihitajika kulipa Sh 500 bilioni na endapo watachelewesha wanatakiwa kulipa faini.
“Sheria iliyopo mzabuni wa ndani anatoa kwanza mzigo malipo yake yanakuja baada ya kusambazwa kwa dawa lakini yule wa nje analipwa asilimia 80 ndipo analeta mzigo,”amesema Magita.
Kutokana na utaratibu huo wamejikuta wanazalisha bidhaa na kujilimbikizia madeni na hivyo wanashindwa kuagiza malighafi kwa kukosa fedha.
Aidha, Magita alibanisha changamoto zingine ambazo zimekuwa zikiwakabili wazalishaji wa dawa ni pamoja na mkanganyiko wa taasisi za Serikali katika ukaguzi na utoaji vibali, tozo za kuingiza malighafi, mazingira ya uhifadhi malighafi bandarini na uhaba wa dola.
Pia ameongeza kuwa, kumekuwa na kero ya katizo la umeme na maji hali ambayo ni kikwazo kikubwa katika uzalishaji wa dawa kwani wamekuwa wakitumia fedha nyingi katika uzalishaji.
“Tunanunua maji lita moja 1, kutoka Wami Ruvu kwa Sh 1 ambapo kisima ni chetu,umeme ni wetu lakini tunatakiwa kutoa kiasi hicho kwa tanki la lita milioni moja ambalo linatumika kwa siku tatu,”amesema.
Nae David Lutabana ambaye ni Meneja wa Ubora Kiwanda cha dawa cha Katwaza, amesema umeme umekuwa ni tatizo kwenye uendeshaji wa viwanda kwani hautabiriki na kusababisha hasara wakati wa utengenezaji wa dawa.
“Baada ya kufuatilia kwa muda tumegundua tunakatiwa umeme pasipokuwa na ratiba walianza kila jumatano mwisho wa siku unakatwa mara mbili au tatu kwa wiki hivyo inatubidi kusimamisha uzalishaji,”amesema Lutabana.
Amesema kama itawezekana wawekewe laini ambayo viwanda vitajitegemea wakati mchakato wa gesi asilia ukiwa unaendelea ambapo wataunganisha ilikuepukana na gharama za mafuta kwenye utumiaji wa jenereta.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Stanslaus Nyongo wakati wa majumuisho amesema kuwa, watakaa kikao na Chama cha wazalishaji dawa nchini (TPMA), Wizara ya fedha, Wizara ya Viwanda na Wizara ya Afya ili kujadili changamoto zilizotolewa.
“Tulishatoa ushauri kwa Serikali lakini leo tumekuja kutembelea viwanda tumekuta changamoto ambazo zimetupa hisia hususani kwenye malipo ya bidhaa kwa MSD na upoteaji wa dola,” amesema Nyongo.
Hata hivyo, Nyongo amesema Serikali inatakiwa kuangalia kwa namna ya kipekee suala la ukosefu wa dola kwani litaweza sababisha upungufu wa dawa nchini ambao utasababishwa kuagizwa kwa malighafi nje ya Nchi.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ