December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawili wadakwa tuhuma za kukutwa na noti bandia akiwemo raia wa Zambia

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe.

JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia wanaume wawili, akiwemo raia wa nchi ya Zambia kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia pamoja na karatasi za kuchapisha pesa bandia lengo likiwa ni kujipatia kipato kwa njia ya utapeli.

Watu hao na wenzao ambao bado wanatafutwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kuunda mtandao wa kutengeneza noti katika mpaka wa Tunduma pia walikutwa na vitambulisho vya Taifa la Zambia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, akizungumza na waandishi wa habari, amesema watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 19, 2023 mtaa wa Mwaka Kati, Mjini Tunduma, Wilayani Momba.

Kamanda Mallya licha ya kutowataja majina watuhumiwa hao kutokana na sababu maalum za kipolisi, amesema watuhumiwa hao akiwemo raia huyo wa Zambia ambae ni Mkazi wa Mpulingu nchini Zambia, walikutwa na noti bandia 12 fedha za Zambia zikiwa zimechapishwa kwa thamani ya kwacha 50.

Amesema watuhumiwa hao pia walikutwa na karatasi 10 zenye ukubwa wa A4 zikiwa zimechapishwa kama kwacha 50 kwa idadi ya noti 36, pamoja na karatasi nyingine moja iliyochapishwa noti nne zenye thamani ya kwacha 100 zikiwa na namba EJ.228951989 na EJ.17714847.

“Lengo la watuhumiwa kufanya matukio haya ni kujipatia kipato isivyo halali na mbinu iliyotumika ni kutengeneza noti bandia kwa kutumia komputa,printa na karatasi za A4,” amefafanua Kamanda Mallya.

Aidha, Kamanda Mallya amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na visu viwili kikubwa na kidogo cha kukunja , mkasi mmoja wa kukatia karatasi pamoja na vitambulisho vya Taifa la Zambia.