Judith Ferdinand-Timesmajira Online-Mwanza
Watu wawili wanadaiwa kufa maji katika matukio mawili tofauti likiwemo la mvuvi kuzama majini ndani ya Ziwa Victoria mtaa wa Bushata kisiwani Bezi Kata ya Kayenze wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Akizungumza mkoani hapa,Machi 1,2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,amesema tukio la kwanza liliyokea Februari 24,2026, majira ya saa mbili usiku,mtaa wa Bushata Bezi, Kata ya Kayenze, Wilaya ya Ilemela,ambako Abubakari Ramadhan(44), mvuvi na mkazi wa eneo hilo, alizama majini na kupoteza maisha alipokuwa akiendelea na shughuli zake za uvuvi.
Mutafungwa,amesema marehemu huyo kabla ya kukutwa na mauti alikuwa akitumia mtumbwi usio na usajili wala jina la mmiliki. Mwili wake ulipatikana Februari 25,2026 ukiwa unaelea pembezoni mwa fukwe za Ziwa Victoria eneo la Bushata kisiwani Bezi.
“Baada ya uchunguzi wa kitabibu kukamilika na utambuzi kuthibitishwa, mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi,”amesema Mutafungwa.
Katika tukio jingine, Mutafungwa alisema,Machi 1,2026 majira ya saa mbili asubuhi, katika mtaa wa Mtakuja, Kata ya Nyamh’ongolo, Wilaya ya Ilemela, ulipatikana mwili wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 hadi 50.Â
Mwili huo ulikutwa katika shamba la miwa lililopo kwenye bonde la mto maji ya rangi ambapo uchunguzi wa awali umeonesha kuwa marehemu huenda alisombwa na maji kutoka eneo jingine kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, hali iliyomfanya ashindwe kuhimili nguvu ya maji.Â
Mutafungwa amesema,mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu na taratibu za utambuzi.
“Kutokana na matukio haya na kuendelea kwa mvua za masika,natoa rai kwa wananchi kuepuka kuvuka mito, mifereji na mabonde yenye maji yanayotiririka kwa kasi pia kutoingia ziwani au kufanya shughuli zisizo za lazima majini wakati wa hali mbaya ya hewa ili kuepusha majanga yanayoweza kuzuilika,”amesema Mutafungwa.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria