Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na bunduki moja aina ya Shotgun Pump Action bila kibali .
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Benjamin Kuzaga amesema hayo Mei 15,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana tukio hilo ambapo amesema Aprili 29,2024 Majira ya usiku huko Nzovwe Jijini Mbeya walivunja jengo la Black Microfinance na kuiba silaha hiyo.
Hata hivyo Kamanda Kuzaga amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Nerbat Bwiga (33)mkazi wa Ifumbo mwingine ni Isaya Zumba (38)mkazi wa Airport Songwe wote ni wakazi wa Mkoa Mbeya.
Kamanda Kuzaga ameongeza kuwa, kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi kupitia kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na uhalifu lilifanya ufuatiliaji ambapo Mei 11, 2024 huko Kijiji cha Itete kilichopo Kata ya Isuto mkoani Mbeya lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Nerbat Bwiga akiwa na silaha hiyo.
Aidha, Kamanda Kuzaga amesema kuwa mtuhumiwa amekiri kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu kwa kushirikiana na mwenzake Isaya Zumba.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kutafuta kazi halali ya kufanya na kuachana na uhalifu kwani hauna nafasi huku likiwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi