November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawili mbaroni kwa tuhuma za kujifanya maofisa wa Jeshi la Polisi

Na Esther Macha , Timesmajira Online, Mbeya

WAKAZI wawili wa Songea mkoani Ruvuma wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za kujifanya Maofisa wa Jeshi la Polisi Tanzania na kumtishia mkazi wa Mbalizi aitwaye Meck Mpepo na kumpora fedha taslimu shilingi 700,000 pamoja na simu tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 5,2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya , Benjamin Kuzaga amesema waatuhumiwa walikamatwa katika Mji mdogo wa Mbalizi maeneo ya Stendi ya Tunduma katika misako inayoendelea.

Ambapo watuhumiwa hao walijifanya maofisa wa polisi walimkamata Meck Mpepo na kujitambulisha wao kuwa ni askari polisi kisha kumnyanganya fedha taslimu 700,000 pamoja na simu tatu.

Kamanda Kuzaga amewataja watu hao kuwa ni Juma Mapunda (47),Said Wanyika (27) ambao wote ni wakazi wa Songea mkoani Ruvuma ambao walijifanya kujifanya maafisa wa jeshi la polisi Tanzania .

Hata hivyo Kuzaga amesema watuhumiwa wamehojiwa na kukiri kufanya matukio kadhaa ya utapeli katika mikoa ya Mbeya,Songwe na Ruvuma kwa kujitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi.

Mkazi wa Iyunga jijini Mbeya , Boni Sanga amesema kuwa watu kama hao wamekuwa wakijitokeza katika jamii hivyo amelipongeza jeshi la polisi kwa jitihada hizo na kuwaomba wananchi wenye taarifa za watu kama hao kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kwani wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya wananchi .