Judith Ferdinand,Timesmajira,Online, Morogoro
SERIKALI imewataka wadau wa uwekezaji nchini kugeukia Sekta ya Mifugo hasa katika kutumia fursa ya changamoto ya uhaba wa mbegu za malisho ambayo mahitaji yake ni zaidi ya tani milioni 7 kulinganisha uzalishaji wa sasa wa tani 127 pekee.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akifungua warsha maalum ya wadau wa uzalishaji mbegu za malisho hapa nchini yaliyofanyika mkoani Morogoro jana Mei,12 mwaka huu.
Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kiwango cha uzalishaji wa mbegu ni mdogo ukilinganisha na mahitaji yake na kwamba kama wawekezaji wakigeuza changamoto hiyo kuwa fursa inasadia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji.
“Mahitaji ya mbegu za malisho Tanzania ni tani milioni 7 lakini kiwango cha mbegu kilichozalishwa kwa mwaka 2019/20 ni tani 127 maana yake ni kwamba kuna uhaba mkubwa sana hivyo changamoto hiyo tuichukulie kama fursa ya uwekezaji katika sekta hiyo,” amesema Prof Gabriel.
Pia amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, makampuni na watu binafsi wenye nia ya kuzalisha mbegu bora za malisho, kufanya kazi hii kibiashara kwa kuwapa mwongozo unaostahili.
Amebainisha kuwa lengo ni kufanikisha juhudi hizi za serikali hasa kujiletea faida za kiuchumi kupitia uwepo wa fursa ya wingi wa mifugo nchini na hata kuuza malisho katika mataifa mengine.
“Hii si tu kwamba itainua uchumi wa mtu binafsi bali italipatia taifa fedha za kigeni, hasa tukizingatia kuwa wananchi wanaweza kutumia fursa ya ardhi iliyopo kuzalisha malisho kibiashara kama wanavyo zalisha mazao ya chakula,”. amesema Prof. Gabriel.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Utafiti,Mafunzo na huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa amesema lengo la warsha hiyo ni kuhakikisha tafiti zilizofanyika kubaini mbegu bora za malisho zinawafikia wafugaji wadogo kwenye mashamba yao.
Amesema zipo mbegu ambazo zimekuwa rahisi kuwafikia wafugaji kama mbegu aina ya Nyasi, mikunde inayotambaa na mikunde jamii ya miti malisho ambazo zipo katika makundu tofauti ambazo pia mahitaji ya msingi katika mashamba ya malisho.
“Tunaona kuna fursa kubwa ya uzalishaji wa mbegu endelevu na hapa tunazungumzia mbegu mafungu matatu ambazo hizo tunaangalia ni namna gani tunaongeza uzalishaji hapa nchini” amesema Dkt. Mwilawa.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam