Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, amewakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza mkoani Songwe kwa kuwa Mkoa huo umedhamiria kuvutia uwekezaji kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Ametoa wito huo Januari 30, 2024, wakati akielezea hali ya maendeleo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu maalumu ya tumekusikia, tumekufikia inayoendeshwa na Idara ya Habari Maelezo.
Programu hiyo kwa pamoja iliwakutanisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vilivyopo mkoani hapo, watendaji wa serikali wakiwemo wakurugenzi wa Halmashauri zote tano za Mkoa, pamoja na Wakuu wa taasisi za umma.
Dkt. Michael amewakaribisha watu wenye mitaji kuja kuwekeza katika sekta za viwanda,kilimo,bandari na madini kwa kueleza kuwa Mkoa unahitaji kufungua zaidi sekta hizo ili kurahisisha maendeleo ya kijamii na uchumi.
Amesema Mkoa huo umepima viwanja 15 kwa ajili ya viwanda vikubwa, viwanja 16 kwa ajili ya viwanda vya kati pamoja na viwanja vingine 16 kwa ajili ya viwanda vya kawaida.
Aidha, Dkt. Michael amesema kuna fursa kubwa kwa wawekezaji katika sekta ya kilimo hususani uzalishaji wa mbolea kwa kuwa tayari kuna malighafi ya kutosha kama atapatikana muwekezaji kwa ajili ya kuzalisha mbolea.
“Katika eneo la Ngwala Wilaya ya Songwe kuna mgodi mkubwa wa madini adhimu (rare earth) kwenye mgodi huo kunapatika madini ambayo ni malighafi kwa ajili ya mbolea hivyo kuna fursa wawekezaji njooni,”amesisitiza Dkt. Michael.
Pia amesema uwekezaji kwenye viwanda vya mbolea katika Mkoa wa Songwe utakuwa na tija kubwa kutokana wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambao ndio wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula kuwa na uhitaji mkubwa wa mbolea, ikiwemo nchi jirani za Zambia Malawi.
Ameongeza kuwa, fursa nyingine ni katika eneo usafirishaji kwa kuwa tayari Mkoa huo umetenga hekari 2000 kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu, kwa kuwa asilimia 70 ya mizigo yote inayoshushwa katika bandari ya Dar es salam upitia Mkoa wa Songwe kwenda katika nchi za Kusini mwa Afrika.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa Dkt.Michael ameeleza mafanikio mbalimbali na kuishukuru serikali kwa kuupatia Mkoa huo fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema mafanikio yaliyoletwa na fedha hizo ni pamoja na sekta ya elimu kunufuika kwa kuongeza ufaulu kutoka asilimia 89.5 mpaka asilimia 90 kidato cha nne na ongezeko la ufaulu kidato cha sita kutoka asilimia 99.8 mpaka asilimia 100.
Aliongeza kuwa, katika sekta ya barabara serikali ilitenga bilioni 39 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambapo kuna ongezeko la kilomita kutoka 206-256 za kiwango cha lami.
Katika program hiyo, nao Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote tano za Mkoa wa Songwe walipata fursa ya kueleza namna walivyosimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi