November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wavuvi waelezea ufanisi,tija wa boti za kisasa za uvuvi

Judith Ferdinand,Timesmajira Online Mwanza

Baadhi ya wavuvi wa Ziwa Victoria mkoani Mwanza walionufaika na boti za kisasa za uvuvi zilizotolewa na Serikali kwa lengo la kutoa ajira na kukuza uchumi wa bluu wameeleza ufanisi na tija walioipata kupitia boti hizo.

Januari 30, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan aligawa boti hizo za kisasa 55 kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa katika hafla iliofanyika jijini Mwanza.

Boti za kisasa za uvuvi katika mwalo wa Mswahili

Wavuvi hao wameeleza kuwa kupitia boti hizo uzalishaji wa samaki umeongezeka kutoka kuvua kilo 20 hadi kilo 300 kwa wiki(siku saba) huku wakiahidi kuwa watarejesha mkopo wa boti hizo bila wasiwasi.

Huku ufanisi mwingine ni kuwa boti hizo zinakifaa kinachoitwa ‘ fish finder’ ambacho kinasaidia kuonesha samaki waliopo pia kinaelekeza mahali unapo toka, kwenda na ulipo hali inayoelezwa kuwa ni rahisi hata kupata msaada endapo itatokea changamoto.

Hayo yamebainishwa Juni 21,2024 na wavuvi hao mara baada ya waandishi wa habari kutembelea baadhi ya wanufaika wa boti hizo katika mwalo wa Mswahili uliopo wilayani Nyamagana jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kikundi cha Tunza Mazingira Mkuyuni wilayani Nyamagana,Charles Lulinga ameeleza kuwa tangu wameanza kufanya kazi ya uvuvi kupitia boti hizo wameweza kutunza akiba ya zaidi ya milioni 3 kwenye akaunti ya kikundi chao.

Ameeleza kuwa awali wavuvi walikuwa awathaminiki kwani waliambiwa ni watu wasiokopesheka,awadhaminiki na ni watu wa kuhamahama na wasiyo na elimu lakini Rais amewaheshimisha kwa kuwapa mkopo wa zana za uvuvi bila dhamana yoyote.

“Awamu hii imemtambua mvuvi na kumkopesha boti hizi ambazo zimetusaidia awali tulikuwa tunatumia boti za kawaida za mbao na baada ya Rais kutuwezesha kupata vitendea kazi ambavyo ni vya kisasa vimesaidia kufanya kazi kwa ubora na usalama zaidi,maslahi pia na kikundi chetu kinasonga mbele,”.

Baadhi ya wavuvi wa mwalo wa Mswahili uliopo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wakiwa wamebeba samaki wakitoka ndani ya boti la uvuvi

Ambapo ameeleza kuwa wakati wa upepo walikuwa wanashindwa kwenda kuvua ili ibidi kuegesha pembeni lakini uzuri wa boti hizi za kisasa inaendelea kufanya kazi huku akieleza kuwa zipo changamoto ambazo haziondoi ubora wa mradi huo.

Mwenyekiti wa BMU Mkuyuni Robert Charles ameeleza kuwa wamepata faida nyingi kupitia boti hizo ikiwemo watu kupata ajira hivyo ameiomba serikali kuendelea kutoa boti hizo kwa wavuvi wa Kanda ya Ziwa kwani zimeleta chachu ya kufanya kazi kwa kufika maeneo ya mbali zaidi ambapo mazao ya samaki yanapatikana kiurahisi tofauti na awali walikuwa wanatumia boti za kawaida ambazo haziwezi kufika mbali.

“Kanda ya Ziwa wavuvi tuwezeshwe zaidi zana hizo za uvuvi za kisasa kwani nchini hapa Kanda hii inategemewa katika pato la taifa na Ziwa Victoria ndilo Ziwa Kuu linalosaidia katika masuala ya uvuvi katika mwalo huu wa Mswahili tuna vikundi vinne ambavyo vimewezeshwa boti hizo na tunaendesha maisha yetu,”.

Naye Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa wavuvi Chembaya kilichopo Halmashauri ya Buchosha Robert Lwanga, ameeleza kuwa kupitia boti hizo wameondokana na changamoto nyingi ambazo walikuwa wanazipata katika shughuli za uvuvi.

“Tumepunguza idadi kubwa ya ajari za kwenye maji,vifo vya wavuvi vilikuwa vinasababisha na vyombo hafifu lakini kwa sasa watu wanaenda wakiwa katika usalama wa kutosha kwani zinahimili hali ya upepo ziwani, kwenye chama chetu pato limeongezeka kutoka kilogramu 20 mpaka 300 kilogramu za samaki kwa siku saba ambapo kwa kilo moja ya samaki ni shilingi 10,000 hivyo katika kilo hizo ni sawa na milioni 3 kwa wiki,tutaweza kurejesha mkopo huo kwani kwa mwezi tunatakiwa kurejesha milioni 1,”ameeleza.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Edwin Mhede

Mwanachama wa Ushirika wa Bukasiga Wilaya ya Ukerewe Tecla Bwire,amesema”Sisi ni wanufaika wa boti ya dagaa,Wizara itusaidie tuweze kupata hata boti tano kwani samaki wanatabia ya kusambaa hivyo boti moja ikikosa nyingine inapata na pia tuwezeshwe nyavu za samaki kwa sababu kipindi ‘tunapaki’ kwenye mbalamwezi basi tuvue sangara ili tusiyumbe kiuchumi,”.

Aidha Msiriakale Juma kutoka chama cha Chembaya FICOS Buchosha,ameeleza kuwa boti hiyo inakifaa kinachoitwa ‘fish finder’ ambacho kina programu mbalimbali na matumizi yake kama simu janja ambacho kinakuelekeza samaki zilipo.

“Ukienda sehemu ya umbali unakitoa kwenye ‘fish finder’ unakipeleka kwenye ‘GPS’ kinakuelekeza kuwa sasa umetoka hapa unakwenda sehemu fulani kuvua na siku ukiwa unataka kurudi kinakuelekeza ulipotoka na ambaye hafahamu namna ya kukitumia ni vyema aende kwa wataalamu ili wamsaidie”.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Edwin Mhede,ameeleza kuwa serikali haitarudi nyuma katika kuboresha sekta hiyo ambapo itaendeleza mradi.

Huku akieleza kuwa kwa niaba ya serikali ameisha toa maelekezo kwa taasisi zinazohisika za kisekta kuhakikisha changamoto zilizo nje ya uwezo wa wavuvi na zinahitaji utaalamu zinashughulikiwa.

Msiriakale Juma kutoka chama cha Chembaya FICOS Buchosha