March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wavuvi Buchosa wanufaika na mikopo ya TADB

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Buchosa

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),imetoa mkopo wa milioni 705 kwa  vikundi vinne vya wavuvi wa Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza,ikiwa ni moja ya mkakati wa benki hiyo kuongeza uzalishaji wa mazao ya maji nchini.

Pamoja na kuendelea kuimarisha uchumi wa wananchi wanaojihusisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

Ofisa Biashara wa TADB Kanda ya Ziwa,Glacia Marugujo,ameyasema hayo  kwa  waandishi wa habari, waliotembelea  miradi ya vikundi vya Sangara Nyakaliro Ficos na Chama cha Ushirika Chembaya, Desemba 4,2025,katika Kijiji cha Itumbili,Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Glacia, amesema mikopo hiyo inalenga kuyainua makundi ya wavuvi yaliopo Ziwa Victoria, kwa kuwawezesha kuwekeza katika ufugaji wa kisasa wa samaki kwa kutumia vizimba, ambao umeonekana kuwa na tija kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa TADB inatekeleza mradi mkubwa wa uwezeshaji wa vizimba 505 vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 12  eneo la Ziwa Victoria, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuongeza uzalishaji wa samaki na kuongeza kipato kwa jamii zinazozunguka ziwa hilo.

Pia amesema kupitia mradi huo, awamu ya kwanza vimetolewa vizimba 452 vyenye thamani ya bilioni 1.1,  na vimeanza kuchochea ongezeko la uzalishaji wa samaki na kujenga ajira endelevu kwa vijana na wanawake wa maeneo husika.

Amefafanua kuwa tayari kiasi cha tani 401 kimevunwa na vikundi vinne  vya vyama vya ushirika, kikundi cha vijana 15 pamoja na wanawake vilivyokopeshwa sh. milioni 705 huku vikirejesha  sh. milioni 329 za mkopo.

“Uwezeshaji huu ni juhudi za serikali kukuza ufugaji wa vizimba (cage-farming) ndani ya mikoa ya Kanda ya  Ziwa Victoria,  ni mkakati wa kuongeza uzalishaji wa samaki na kukuza ajira.Mradi huu ulizinduliwa mwaka jana  na Rais Samia Suluhu Hassan, unaaendelea kufanya vizuri kama mlivyoshuhudia katika ziara hii,”amesema Glacia.

Aidha  amesema,vizimba 53 vya sh. milioni 801  vipo kwenye hatua za mwisho za kukamilika kwa taratibu za utoaji, vitakabidhiwa kwa vikundi vingine vinavyostahili katika Halmashauri ya Buchosa.

Ameeleza kuwa hadi sasa TADB imewafikia na kuwawezesha wavuvi 1,904, kupitia mikopo nafuu, ujenzi wa miundombinu ya ufugaji wa vizimba, mafunzo ya ujasiriamali na huduma za kitaalamu ili kuhakikisha miradi yao inakuwa endelevu na yenye tija.

“TADB itaendelea kuwekeza katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa mazao ya maji ukiwa mkakati wake wa kuchochea maendeleo ya kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda,”amesema Glacia.

Kwa upande wao baadhi ya wavuvi  walionufaika wamesema kuwa, ufugaji wa vizimba umekuwa chanzo kipya cha uhakika wa kipato ikilinganishwa na uvuvi wa jadi, ambao unategemea msimu na mara nyingi huwa na changamoto za kupungua kwa samaki.

Mmoja wa wanachama wa kikundi cha Chembaya, Charles Mafuru, amesema uwekezaji huo wa TADB umeanza kubadilisha maisha ya jamii ya Buchosa kwa kuongeza kipato cha kaya,ajira kwa vijana na kuongeza upatikanaji wa kitoweo cha samaki katika soko la ndani na nje ya nchi.

Naye Katibu wa Chama Cha Ushirika cha Chembaya, Msilikale Juma, amesema kuwa wanavutwa kuongeza uwekezaji katika ufugaji wa samki kwa vizimba kutokana na tija iliyopatikana kupitia uwekezaji huo wa kisasa kulinganisha na uvuvi wa asili.

“Bado hatujakidhi mahitaji ya soko la ndani kutokana na ukubwa, hivyo watu waje wawekeze katika sekta hii ili kuweza kukidhi mahitaji  na kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi,”amesema.