January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wavu waanza kujifua kuelekea Olimpiki

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KIKOSI cha timu ya Taifa ya wanaume ya Wavu ufukweni kimeingia kambini na tayari kimeanza rasmi kujifua kuelekea kwenye michuano ya Kombe la Afrika itakayoanza kutimua vumbi Juni 21 hadi 28, 2021 katika mji wa Agadir nchini Morocco.

Michuano hiyo pia itatumika kwa ajili ya kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Olimpiki, itakayofanyika Tokyo, Japan kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8, 2021.

Awali michuano hiyo ilipangwa kufanyika Machi 26 hadi 30 katika fukwe za Coco lakini yaliahirishwa kutokana na mlipuko wa Covid-19 na kabla ya kuahirishwa kwa mashindano hayo, Shirikisho la Mpira wa Wavu Barani Afrika (CAVB) liliiteua Tanzania kuwa mwenyeji.

Mbali na sasa Morocco kuwa mwenyeji, nchi zingine zitakazoshiriki mashindano kwa upande wa wanaume ni Benin, Botswana, Congo Brazzaville, Egypt, Ghambia, Ghana, Ivory Coast, Kenya, Mali, Mauritius, Mozambique, Niger, Nigeria, Rwanda, Sierra Leone, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Togo, Tunisia, Zambia na Zimbabwe.

Kwa upande wa wanawake zipo Cape Verde, Egypt, Gambia, Ghana, Ivory Coast, Kenya, Mauritius, wenyeji Morocco, Mozambique, Niger, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda, Sierra Leone, Afrika Kusini Sudan na Zambia.

Kikosi kilichoingia kambini kinaundwa na timu mbili ile ya kwanza ikiwa na David Neeke na Ford Edward na timu ya pili inaundwa na Ezeckiel Rabson na Joseph Mafuru na zote zitaendelea kunolewa na Kocha Alfred Selengia ambaye pia ni mkufunzi wa makocha wa wavu wa ufukweni wa Shirikisho la mpira wa wavu Barani Afrika – CAVB.

Akizungumza na Mtandao huu, kocha Selengia amesema kuwa, wamepania kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwenye hatua ya awali za mashindano ya Kanda ya Tano, yaliyofanyika Entebe, Uganda Disemba 2019 ambapo walifanikiwa kushinda mechi zake zote na kupata nafasi ya kusongambele kama vinara katika hatua ya mwisho kombe la Afrika.

Amesema, toka awali walishaweka mkakati wa kufanya vizuri katika michuano hiyo na watahakikisha wanaanza na michuano hiyo ya Kanda ya Tano ya Afrika ya Wavu Ukukweni hatua ya pili itakayotumika kutafuta nafasi za kufuzu kushiriki mashindano ya Olimpiki ‘Africa Sub Zonal V Olympic Qualifiers’.

Kocha huyo amesema kuwa, kwa sasa wanachokisubiri ni kutoka kwa ratiba ya makundi ambayo itapangwa kulingana na ubora wa kila nchi kalingana na orodha ya viwango ya timu bora Afrika.

Ikumbukwe kuwa, kikosi cha Tanzania kilichokuwa kinaundwa na Ford Edward na David Neek huku kile cha pili kikiundwa na Shukuru Ally na Said Alhaj kilifanikiwa kufuzu hatua hiyo ya pili baada ya kufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya awali yaliyofanyika katika fukwe za Lido zilizopo Entebbe, Uganda kuanzia Desemba 18 hadi 22, 2019.

Ushindi walioupata Tanzania dhidi ya Uganda, Kenya na Sudan kuliwafanya kukaa juu ya msimamo wa kundi lao wakifuatiwa na Kenya ambao nao walifuzu kutinga hatua ya pili huku Sudan wakishika nafasi ya tatu na Uganda wakikaa nafasi ya mwisho.