Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Waumini wa Kikristu wamehimizwa kuzingatia mambo ishirini kipindi hiki cha Kwaresma ili kugeuza mienendo mibaya, kuwa wavumilivu na wanyenyekevu.
Wito huo umetolewa Februari 18,2026 wakati wa Misa ya Jumatano ya Majivu na Mchungaji Emmanuel Muhangwa,wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT),Ushirika wa Makedonia Mjimwema, Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria,iliyofanyika kanisani hapo.
“Kwaresma ya mwaka huu ikalete tofauti maishani mwetu kwa kugeuza mienendo yetu mibaya,tupate kibali cha kuuona uso wa MUNGU, baada ya maisha yetu hapa duniani,”amesema Mchungaji Muhangwa.
Mchungaji Muhangwa,amesema kipindi hiki cha kukumbuka mateso ya Yesu, kwa kanisa ni wakati wa kutafakari matendo yao kwa sala,toba kufunga kama yanavyosema maandiko matakatifu.
Akirejea maandiko hayo kutoka kitabu cha Nyakati wa pili,sura ya 7 na mstari wa 14,isemayo,”Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekeza, kuomba, kunitafuta uso na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi zao, na kuiponya nchi yao,”.
Amesema kipindi hiki cha Kwaresma,waumini wa Kikristu wanapaswa kuzingatia baadhi ya mambo wakati wa kufunga ikiwa ni pamoja na kufunga dhambi ili wapate utakatifu na kuweza kutafuta uso wa Mungu.
Pili kufunga huzuni ili wapate furaha,kufunga majivuno wapate utukufu kwa kuacha kujisifu wenyewe,kufunga wivu wapate baraka kutoka kwa Mungu, kufunga kinyongo wapate faraja na kuondokana na changamoto ya msongo wa mawazo.
Pia amesema,wanapaswa kufunga uchoyo wapate neema kwani wanatamani kuishi maisha ya ushirikiano na kujaliana katika kipindi hiki cha Kwaresma na wakati wote wa maisha hapa duniani.
Kufunga dharau wapate heshima,kufunga hofu wapate imani,kufunga kiburi wapate unyenyekevu,kufunga hasira wapate upole na kufunga ujinga wapate hekima.
“Neno la Mungu linasema kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa bali wapumbavu hudharau hekima na adabu, pia neno la Mungu ni taa ya maisha yetu kwa hiyo tunapo soma neno la Mungu na kujaa mioyoni mwetu tutapata hekima, na kutembea katika njia iliyo nyoofu,”amesema Mchungaji Muhangwa.
Lakini pia kufunga umbea wapate amani,kwani mara nyingi umbea huleta mifarakano na kukosesha amani katika maisha ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, amewataka kufunga matusi ili wapate uchaji,kufunga aibu wapate ujasiri.
“Kuishi maisha ya aibu kunaweza kusababisha mtu akafanya vitu visivyompendeza Mungu katika jamii pamoja kukosa ujasiri wa kutembea au kukemea jambo ovu linalotokea katika jamii au taifa,”amesema Mchungaji Muhangwa.
Vilevile,amewataka waumini hao kujikita katika kufunga chuki wapate marafiki,chuki hupunguza marafiki ambao ni msingi wa maisha ya mwanadamu kamili kwani msingi wa mtu ni watu pamoja na kuwa na ushirika na watu.
Aidha,amewataka kufunga uvivu ili wapate mafanikio kwani uvivu ni dhambi hata biblia imesema asiyefanya kazi na asile, hivyo wafanye kazi kwa bidii pamoja na kufunga ulevi ili wapate afya,kwani watu wengi wameharibu afya zao kwa vitu vya starehe na ulevi.
Kadhalika amewaasa kutumia kipindi hicho cha Kwaresma kufunga uzinzi ili wapate wongofu na katika kukumbuka mateso ya Yesu Kristu uzinzi haukubaliki kwani Mungu hapendi na inachangia kukosa hofu.
Huku jambo la kumi na tisa ambalo wakristu wanapaswa kuzingatia kipindi hiki cha Kwaresma ni kufunga roho mbaya wapate upendo pia, kufunga starehe wapate muda wa sala.
“Watu wengine wameacha muda wa sala na ibada na kujikita katika starehe,ukiangalia haya mambo 20 nilioyasema,ni vizuri kuishi katika maisha matakatifu na kutafakari matendo yetu na yale yasiyo mtukuza Mungu tuyaache,”amesema Mchungaji Muhangwa.
Kwa upande wake mmoja wa waumini wa Kanisa hilo,Bertha Rock,amesema katika kipindi hiki cha Kwaresma wanapaswa kukitumia kuomba toba na rehema za Mungu ili yaliyotokea Oktoba 29,mwaka jana yasijirudie.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama