February 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waumini Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki wamlilia Rais Dkt.Samia

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WAUMINI wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (K.K.A.M) Kata ya Makwale wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya wamemuomba
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwasaidia wasizuiliwe kuabudu Kwenye makanisa waliyojenga kwenye Kaya zao.

Akizungumza na TimesMajira mmoja wa waumini wa kanisa hilo kata ya Makwale Elen Msopa, amedai  watu ambao wanawazuia kuabudu kwenye makanisa yao hawajulikani kama wapo kwenye Kaya zao na kama wapo basi waonekane wafahamike.

Inadaiwa kuwa bodi ya wadhamini wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dayosisi ya konde ndio wanawazuia waumini wa kanisa la K.K.A.M kuabudu kwenye maeneo yao bila kuainishwa sababu za msingi juu ya haki hiyo ya uhuru wa kuabudu.

Msopa amesema kuwa shauri la ardhi namba 24 la mwaka 2023 katika baraza la ardhi na nyumba wilaya ya Kyela lilitupiliwa mbali na Mwenyekiti wa Baraza na kuelekeza upande usioridhika na uamuzi wa baraza ukate rufaa ndani ya siku 30 lakini badala ya kukata rufaa  waliambiwa wasimame kuendelea na ibada katika makanisa hayo.

“Tunashangaa kimetokea nini cha kutaka tuondolewe kwenye makanisa yetu wakati shauri namba 24 la ardhi la mwaka 2023 ile hukumu ilitupa ushindi sisi (KKAM). Tunamuomba Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan atusaidie, maeneo haya ni asili yetu twende wapi sasa”, amesema Msopa.

Muumini mwingine wa usharika wa Isimba  kata ya Makwale Tupokigwa Kisisiri, amesema alizaliwa mwaka 1969 na kukuta kanisa lipo  na kuonyesha kushangazwa na watu wanaojitokeza kusema makanisa hayo ni yao.

“Tunaomba Mhe.Rais Dkt.Samia utusaidie maana kanisa hili ni mji wetu hatukuchanga hela na kwamba sio kwamba Dayosisi ilitusaidia kuchanga fedha huu ni Mji wa mzee wetu Andamwile na kujenga amejenga mtoto wetu wala hatukuona mchango wowote  tunaomba Mhe. Rais upokee kilio chetu maana tunakuja kuvamiwa maana nchi yetu ni ya amani tunalia”, amesema Kisisiri.

Eliezery Ngailo kutoka usharika wa Ngeleka amesema kuwa  maeneo yote yaliyojengwa makanisa walipewa na mababu zao lakini cha ajabu suala limegeuka kuwa shida kwao na kufanya sehemu ya kuabudia kwao kuwa changamoto na kufanya kuishi kama wakimbizi licha ya kuwa maeneo hayo kuwa yao.

Aston Mwalundilin kutoka usharika wa Eden amesema kwamba eneo hilo lilipatikana mwaka 1968 wakati walifikiri wapo wajenge eneo la Kanisa na  kuwafikia wazee wawili na kukubaliana kuwapatia eneo kwa  ajili ya kuabudu na kugawa eneo lenye ukubwa wa robo tatu heka(Ekali).

Akizungumzia sakata hilo  Katibu Mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Konde, Benjamin Mbembela amesema kuwa amri ilitolewa waumini wa K.K.A.M na KKKT tumie makanisa hayo lakini cha ajabu wenzetu bado wanatumia makanisa hayo .

“Kesi hii iliondolewa  kwa mapungufu ya kisheria mahakamani na na madai ya kusema sisi tumewazuia sio kweli,lakini kitu kingine wao walipoitwa walidai wanaohusika si wao hivyo ikabidi wakili wa K.K.A.M apeleke shtaka lingine “amesema.