Na Moses Ng’wat, Timesmajira, Online Ileje.
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Songwe umewashitaki kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri watumishi sita (6) ambao wamebainika kufoji vyeti vya ndoa kwa kupeleka wenza feki kwa lengo la kupata huduma za matibabu kupitia mfuko huo kinyume cha sheria.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa mfuko huo, Mkoa wa Songwe, Simon Mmbaga, wakati akiwasilisha mambo ya muhimu kuhusiana na mfuko wa bima ya afya, ikiwemo kuwaomba madiwani kama viongozi wa jamii kusaidia kuelimisha wananchi kuhusu kujiunga na mfuko katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Mmbaga ameeleza kuwa, baada ya NHIF kufanya utafiti kwa kupitia mifumo ya mfuko huo kwa Mkoa wa Songwe walibaini watumishi 6 waliwachukua kaka na dada zao na kuwapeleka ofisi za wakuu wa Wilaya na kuwatambulisha kuwa ni wenza wao ili waweze kupatiwa vyeti vya ndoa.
“ Naomba kutumia nafasi hii kuwaomba sana viongozi wangu (Madiwani) mtusaidie kukemea vitendo kwani udanganyifu ni mkubwa sana, kibaya zaidi baadhi ya watumishi wamekuwa wakitengeneza ndoa feki na kaka au dada zao ili ndugu hao nao waweze kukidhi vigezo na masharti ya mfuko na kupatiwa matibabu kinyume cha sheria,” alieleza Mmbaga.
Amesema kuwa watumishi hao waliamua kufanya udanganyifu huo ili kuwezesha ndugu zao hao kukidhi vigezo na masharti ya mfuko ikiwemo kuwasilisha vyeti vya ndoa na nyaraka nyingine za kiutumishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Nuru Kindamba, amekiri watumishi wake wawili kubainika kufanya udanganyifu kwenye mfuko huo kwa kuwaingiza ndugu zao ambao hawatambuliwi kisheria na mfuko huo.
“Kwenye baraza letu tuliwaalika wenzetu kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kuja kutuelezea mambo mbalimbali, na kama mlivyosikia kwenye taarifa yao wameeleza kuwa kuna watumishi wetu wawili (Halmashauri ya Wilaya ya Ileje) wamefanya udanganyifu kwenye mfuko”.
Kindamba amesema ni kweli suala hilo lipo ofisini kwake na tayari taratibu za kiutumishi zimeanza kuchukuliwa , ikiwemo watumishi hao kuamuliwa kurejesha fedha.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi